📍 Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza watangulizi wake kwa mchango wao katika kutekeleza azma ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, akisema kukamilika kwa miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba ni matokeo ya maono yaliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza , Oktoba 30, 2026, jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa majengo na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba, Rais Samia alisema wazo la kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma lilipendekezwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1983, likizingatia nafasi ya kijiografia ya mji huo uliopo katikati ya nchi.
Alisema hatua hiyo ililenga pia kusogeza huduma za Serikali karibu na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Rais Samia aliwataja marais walioendeleza azma hiyo kuwa ni Hayati Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin William Mkapa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambao kwa nyakati tofauti walichangia katika kufanikisha mpango huo.
Hata hivyo, alitoa pongezi za pekee kwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, akisema uamuzi wake wa mwaka 2016 wa kuhamishia shughuli za Serikali jijini Dodoma uliharakisha utekelezaji wa maono hayo.
Alieleza kuwa Aprili 13, 2019, Hayati Magufuli alizindua Mji wa Serikali Mtumba, kufuatia kukamilika kwa majengo ya awali yaliyowezesha wizara, ofisi na taasisi mbalimbali za Serikali kuanza shughuli zake katika eneo hilo, lililokuwa likijulikana kwa jina la Magufuli City.
Rais Samia alisema tangu alipokabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi mwaka 2021, Serikali yake imeendelea na utekelezaji wa mradi huo kwa kujenga majengo ya kudumu ya ghorofa, barabara za lami na miundombinu mingine muhimu kwa ajili ya kurahisisha shughuli za kiutawala.
Alisema mafanikio yaliyofikiwa ni matokeo ya juhudi za pamoja za viongozi na watendaji wa Serikali walioshiriki katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo, huku akiwapongeza Watanzania kwa hatua hiyo ya maendeleo.
Katika uzinduzi huo, Serikali imeweka rasmi katika matumizi majengo 26 ya wizara, majengo 11 ya taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 59.1 na miundombinu mingine iliyojengwa katika eneo hilo.
Kukamilika kwa miundombinu hiyo kunatarajiwa kuimarisha uratibu wa shughuli za Serikali, kuongeza ufanisi katika utendaji wa taasisi za umma na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, mradi huo unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii jijini Dodoma kupitia ukuaji wa biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa za ajira.
Hatua hiyo inaashiria mwendelezo wa utekelezaji wa azma ya muda mrefu ya kuwa na makao makuu ya Serikali yenye miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji ya kiutawala na kuweka mazingira bora ya utendaji kazi.

