Mwanzilishi Mwenza wa Miss Bantu Tanzania ,Season One ,Jackline Kessy akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo


Jaji na Mwalimu wa mashindano hayo ,Lisa Stephen akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mashindano hayo .
…….
Na Happy Lazaro, Arusha
WAANDAAJI wa mashindano ya Miss Bantu Tanzania wametangaza kuwa mshindi wa kwanza wa msimu wa kwanza atazawadiwa gari, fedha taslimu pamoja na tiketi ya VIP ya kuhudhuria mechi ya ufunguzi wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, huku washiriki watakaoshika nafasi ya pili hadi ya kumi wakipatiwa zawadi za fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mwanzilishi Mwenza wa Miss Bantu Tanzania ,Season One ,Jackline Kessy amesema mashindano hayo yameanzishwa kwa lengo la kuenzi utamaduni wa mwanamke wa Kiafrika, kukuza nafasi yake kiuchumi na kijamii pamoja na kuhakikisha maadili na mila za Kiafrika zinaendelezwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema kuwa,wanawake wenye umri wa miaka 18 hadi 45 wanakaribishwa kushiriki mashindano hayo ambapo usajili rasmi utaanza novemba 10 mwaka huu katika viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha .
Kessy amesema Miss Bantu inalenga kutoa nafasi kwa wanawake kujivunia maumbile yao ya asili bila kubaguliwa kwa misingi ya urefu au umbo, akieleza kuwa mashindano hayo yatakuwa tofauti na mashindano ya urembo yaliyozoeleka kwa kuzingatia pia utambulisho na utamaduni wa mwanamke wa Kiafrika.
“Tunakusudia kuhamasisha uhifadhi wa mavazi ya asili, vyakula, ngoma, michezo na lugha za Kiafrika, huku wakisisitiza umuhimu wa kulinda mila na desturi zinazochangia kuimarisha umoja na mshikamano katika jamii.”amesema Kessy.
Aidha, amesema mashindano hayo yanalenga kumwezesha mwanamke kutumia vipaji na fursa zilizopo kujitegemea kiuchumi, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuwa mfano bora kwa wanawake wengine katika jamii.
Kessy amesema kuwa,wanatarajia kushirikiana na wadau husika kutoa elimu na kusaidia juhudi za kukabiliana na changamoto za saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti, ikiwa ni sehemu ya mipango ya kugusa maisha ya wanawake kupitia mashindano hayo.
Kessy amesema mbali na kuenzi utamaduni, Miss Bantu inatarajiwa kuchangia kukuza utalii kwa kutangaza vyakula, mavazi na urithi wa Kiafrika, pamoja na kutoa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira na masuala mengine yanayoigusa jamii.
Kessy amewaalika wadau mbalimbali, wakiwemo taasisi za serikali, kampuni binafsi, wafanyabiashara na watu binafsi, kujitokeza kudhamini mashindano hayo kwa kuchangia mavazi ya asili, vyakula, sanaa na shughuli nyingine zinazohusiana na utamaduni wa Kiafrika.
Kwa upande wake Afisa michezo na utamaduni halmashauri ya jiji la Arusha ,Benson Maneno ,akikabithi kibali cha usajili wa mashindano hayo kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa ajili ya kuendesha Miss Bantu Tanzania ambapo amesema kitatumika kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Maneno amesema kibali hicho ni hatua muhimu katika kuhakikisha mashindano hayo yanaendeshwa kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa, huku akieleza kuwa Miss Bantu ina nafasi ya kukuza sanaa na utamaduni wa Tanzania na kupanua wigo wake kutoka Arusha hadi maeneo mengine nchini.
Ameipongeza taasisi hiyo kwa kufanikisha mchakato wa kupata kibali na kuwataka waandaaji kutumia fursa hiyo kuendeleza utamaduni wa Kiafrika na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukuza shughuli za sanaa na utalii.
Kwa upande wake, Jaji na Mwalimu wa mashindano hayo ,Lisa Stephen amesema Miss Bantu inalenga kusherehekea mwili wa mwanamke wa Kiafrika kwa kuondoa mitazamo finyu inayohusisha urembo na urefu au maumbo fulani ya mwili.
Amesema kuwa,mashindano hayo yatakuwa na fursa mbalimbali za ajira kwa washiriki, ikiwemo kupata mafunzo, kushirikishwa na kampuni na taasisi mbalimbali pamoja na kuwa mabalozi wa bidhaa na huduma (brand ambassadors).
Lisa ameongeza kuwa, kupitia ushirikiano na wadau na wafadhili, washiriki watapata nafasi ya kutumia vipaji na umaarufu watakaoupata kujipatia kipato, huku wakijenga uwezo wa kujitegemea.
