Makamu Mkuu wa Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Apollinary Kamuhabwa, leo Oktoba 27, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kongamano la 18 la Utafiti la MUHAS

 Daktari bingwa wa watoto, Profesa Karim Manji akizungumza na waandishi wa habari umuhimu wa utafiti

…………

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Serikali imesema itatumia matokeo ya tafiti za kisayansi kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga, hususan waliozaliwa kabla ya wakati na wenye uzito mdogo, ili kupunguza vifo na kuwawezesha kukua katika mazingira salama.

Akizungumza leo Oktoba 27, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kongamano la 18 la Utafiti la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), lililolenga kujadili matokeo ya tafiti na mchango wake katika kuboresha huduma za afya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe.

Amesema Wizara ya Afya itatumia matokeo ya utafiti kuhusu huduma za ulishaji wa watoto wachanga kuimarisha miongozo ya kitabibu, kuboresha usaidizi wa unyonyeshaji na kuzuia maambukizi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi.

Dk Magembe amesema watoto wachanga wanachangia takribani nusu ya vifo vyote vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, hivyo kuimarisha huduma katika siku za mwanzo za maisha ni muhimu katika kupunguza vifo hivyo.

Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kusisitiza umuhimu wa unyonyeshaji na huduma ya Kangaroo Mother Care, inayohusisha kumweka mtoto ngozi kwa ngozi na mama yake, hasa kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati au wenye uzito mdogo.

Aidha, amewataka wazazi na walezi kuachana na dhana potofu kuhusu ukamuaji wa maziwa ya mama, akieleza kuwa watoto wasioweza kunyonya moja kwa moja wanaweza kulishwa maziwa hayo kwa njia salama zinazoshauriwa na wataalamu wa afya.

Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Apollinary Kamuhabwa, amesema tafiti za vyuo vikuu zinapaswa kuleta mabadiliko yanayoonekana katika utoaji wa huduma kwa jamii badala ya kubaki katika machapisho ya kitaaluma.

Amesema ushirikiano kati ya MUHAS na taasisi za kimataifa, ikiwamo Chuo Kikuu cha Harvard na washirika wa utafiti kutoka Sweden, ni muhimu katika kuzalisha ushahidi wa kisayansi unaoweza kutumika kutatua changamoto za afya nchini.

Ameongeza kuwa matokeo ya utafiti huo yanatarajiwa kusaidia kuboresha huduma za ulishaji wa watoto wachanga, kuongeza ujuzi wa wahudumu wa afya na kuimarisha msaada kwa kina mama wenye watoto wanaohitaji uangalizi maalumu.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, daktari bingwa wa watoto, Profesa Karim Manji, amesema utafiti wa Low Birth Infant Feeding Exploration (LIFE), uliofanyika Tanzania, India na Malawi, ulibaini changamoto mbalimbali katika utoaji wa huduma kwa watoto wachanga.

Amesema nchini Tanzania utafiti huo ulifanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Amana na Hospitali ya Temeke, ambako changamoto zilizobainika ni pamoja na kuchelewa kuanza kunyonyesha, ushauri usiotosheleza kwa kina mama na udhaifu katika utunzaji wa kumbukumbu za kitabibu.

Profesa Manji amesema ni asilimia tano ya watoto wachanga waliohusishwa katika utafiti huo waliopata maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa, huku asilimia 44 ya kina mama wakipata aina fulani ya ushauri kuhusu unyonyeshaji.

Amesema matokeo hayo yanaonesha umuhimu wa kuongeza msaada wa vitendo kwa kina mama, kuboresha ufuatiliaji wa lishe na uzito wa watoto pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya katika kutoa huduma stahiki.