Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba akizungumza kwenye Mahafali ya Tano ya Chuo cha Benki Kuu Mwanza

Wahitimu wa Chuo cha Benki Kuu wakiwa ukumbini
………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wahitimu Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania wamehimizwa kutumia maarifa waliyoyapata kwaajili ya kutafuta suluhisho za changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta ya fedha.
Hayo yamebainishwa Leo Ijumaa Oktoba 30, 2026 na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba wakati alipokuwa akizungumza kwenye Mahafali ya tano ya Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo hicho Jijini Mwanza.
Amesema katika sekta ya fedha suala la Imani kwa wananchi huwa ni mtaji muhimu sana na imani hiyo hujengwa kwa uaminifu,uadilifu,siri ya kutunza taarifa za wateja pamoja na kuheshimu sheria zilizopo kanuni na taratibu katika usimamizi wa fedha.
Aidha, amewakumbusha wahitimu kuendelea kuwa wabunifu na wachapa kazi ili kwakutumia elimu waliyoipata waweze kuleta maendeleo yao binafsi,jamii na Taifa kwaujumla
Ameeleza kuwa wahitimu wanapaswa kuwa tayari kujifunza teknolojia mpya,kufanya kazi kwaushirikiano na kuendelea kushiriki katika kujenga mazingira mazuri na imara kwenye sekta ya fedha.
Ameongeza kuwa vyeti walivyovipokea leo siyo mwisho wa kujifunza bali ni mwanzo wa safari ya kuendelea kuongeza maarifa kuboresha ujuzi na kuendana na mabadiliko ya taaluma zao.
“Dunia ya sasa inabadilika kwa kasi na maarifa yanayotosha leo inawezekana kesho yasikidhi mahitaji ya soko hivyo tambueni kwamba mnahitajika kujifunza na kujiendeleza kitaaluma kwenye nyanja nyingine”,
Kwaupande wake Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Nicas Yabu amewaomba wahitimu waende wakafanye kazi kwa weledi,uzalendo na kwa maadili mema ili waweze kuwakilisha Chuo hicho vizuri.
Sara Sainyeye ni miongoni mwa wahitimu amesema atatumia elimu aliyoipata kusaidia jamii inayomzunguka hususani kwa wafanyabiashara wadogo kuwaelimisha namna ya kusimamia fedha zao ili waweze kukua kiuchimi.
