Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Majengo, Barabara na Miundombinu muhimu katika Mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma, tarehe 30 Oktoba, 2026.

Akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi waliohudhuria hafla hiyo ya kihistoria, Mhe. Rais amesema kuwa kuzinduliwa kwa Mji wa Serikali Mtumba ni mafanikio makubwa katika mpango wa kuhamishia makao makuu ya serikali na kusogeza huduma muhimu karibu zaidi na wananchi.

 Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza kuwa Wizara na Taasisi mbalimbali kuendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa wananchi.

“Nitoe rai kwenu Watendaji wa Serikali kwamba, pamoja na huduma za Serikali kupatikana hapa Mji wetu wa Serikali Mtumba, bado wananchi hawapaswi kulazimika kuja hapa makao makuu ya nchi kufuatilia kila huduma inayotolewa na Serikali.” Amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan 

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni miongoni mwa Taasisi za Serikali ambazo Ofisi zake zipo ndani ya Mji wa Serikali, Mtumba, ambapo Ofisi inatekeleza jukumu kuu la Utoaji wa huduma za Ushauri Kisheria kwa Serikali Taasisi zake na wananchi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno ni miongoni mwa Viongozi wa Serikali waliohudhuria katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi ambapo kwasasa Ofisi inapatikana katika mikoa takribani 18 nchini.

Pia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa ikiendesha Kliniki za kisheria bila malipo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni jitihada za kutatua changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi