Na Mwandishi wetu, Simanjiro

KERO 102 zimeibuliwa kwenye ziara ya Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Katibu wa Ofisi ya Mbunge wa Simanjiro, Frank Oleleshwa ameeleza hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kilichofanyika mji mdogo wa Orkesumet.

Oleleshwa amesema kero hizo 102 zimeibuliwa na wananchi katika ziara hiyo ya Mbunge wa Jimbo iliyofanyika katika kata nne.

Amesema katika ziara hiyo Mbunge Ole Millya ametembelea na kusikiliza kero, changamoto na kuzungumza na wananchi kwenye Kata za Emboreet, Loiborsiret, Komolo.

Amesema Mbunge huyo alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Emboreet ambapo alizungumza na wanafunzi wa shule hiyo na baadhi ya wananchi wa kata hiyo.

“Baada ya hapo Mbunge alikwenda kwenye kijiji cha Kimotorok Kata ya Loiborsiret ambapo alisikiliza changamoto za wananchi na kisha kuzungumza nao,” amesema Oleleshwa.

Amesema baada ya kijiji hicho aliendelea na ziara yake kwenye kijiji cha Loiborsiret, kisha akamalizia kwenye kata ya Komolo.

Hata hivyo, amemshukuru Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota, kwa kutoa basi na watumishi wakiwemo baadhi ya wakuu wa idara na vitengo kushiriki kwenye ziara ili kujibu kero za watu.

“Katika ziara hiyo Mheshimiwa Mbunge aliwapata nafasi ya kuzungumza wananchi waliokuwa kwenye mikutano hiyo ambapo kero 102 zilitajwa na watu tofauti,” amesema Oleleshwa.

Ametaja baadhi ya kero hizo ni changamoto ya migogoro ya ardhi ambalo linapaswa kupatiwa ufumbuzi.

“Pia kuna changamoto ya baadhi ya barabara zinatakiwa kufanyiwa ukarabati, baadhi ya vitongoji ambavyo bado havijapatiwa umeme na maji,” amesema Oleleshwa.

Amesema pia kuna tatizo la tembo kuvamia makazi katika baadhi ya vijiji ambapo wamesababisha hofu na taharuki kwa watu.

Amesema mbunge ametoa ushauri wa kudhibiti tembo hao kwa kujenga mabwawa karibu na maeneo ya hifadhi ili wakose kitu cha kufuata kwenye makazi ya watu.

“Mheshimiwa Mbunge kupitia nafasi yake ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki hivi sasa yupo nje ya nchi kwenye ziara ya kitaifa, amenituma nije kutoa salamu zake kwenu,” amesema Oleleshwa.