Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na viongozi wa taasisi na makampuni mbalimbali ya Korea Kusini na kujadili fursa za ufadhili, uwekezaji na utaalamu kwa miradi ya kimkakati ya maendeleo Zanzibar.

Mikutano hiyo imefanyika leo, tarehe 30 Oktoba 2026, jijini Seoul, Jamhuri ya Korea (Korea Kusini), na viongozi wa K-FINCO, HEERIM, Sejong Plant, SAMOO C.M. Architects & Engineers pamoja na Sung Shin Rolling Stock Technology Ltd. (SSRST).

Mazungumzo yamelenga kupanua fursa za ufadhili na kuvutia ushiriki wa makampuni ya Korea katika miradi ya kipaumbele Zanzibar, hususan bandari, usafiri wa baharini, barabara, miundombinu ya mijini, nishati mbadala, utalii na viwanda. K-FINCO imeeleza mifumo mbalimbali ya dhamana na ufadhili inayotumika kuwezesha makampuni ya Korea kushiriki katika miradi ya maendeleo.

Mkutano huo pia umejikita katika miradi ya Hospitali ya Rufaa ya Binguni na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar (MICE). HEERIM tayari imeandaa mpango wa maendeleo ya mradi wa MICE, huku taratibu za kumpata mshauri elekezi wa mradi huo wa hospitali zikiendelea. 

Kwa upande wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni, Rais Dkt. Mwinyi amesema mradi huo utahusisha huduma za afya pamoja na mafunzo, hivyo unahitaji vifaa tiba vya kisasa, mifumo bora ya taarifa za hospitali na utaalamu wa usanifu na usimamizi. SAMOO C.M. na washirika wake wamewasilisha uzoefu na uwezo wao katika maeneo hayo.

Katika huduma za maji, mazingira na uchumi wa buluu, Sejong Plant imeonesha nia ya kushiriki katika miradi ya maji safi na salama, usafishaji wa maji taka na mazingira, pamoja na kuangalia njia za ufadhili. Kampuni hiyo pia imeonesha nia ya kuagiza mazao ya uvuvi kutoka Zanzibar na kuwekeza katika mifumo ya uhifadhi kwa baridi ili kusaidia upatikanaji wa soko na kulinda ubora wa mazao hayo.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuendelea kwa mawasiliano ya kitaalamu ili kuchambua miradi iliyojadiliwa, mahitaji yake na mifumo inayowezekana ya ufadhili, kwa kuzingatia taratibu za Serikali na zabuni.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza mpango wa Serikali wa kurejesha huduma ya reli ya abiria na utalii Zanzibar, ambapo Sung Shin Rolling Stock Technology Ltd. imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mradi huo.