Na. Sophia Kingimali, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) anayeshughulikia mazingira, Reuben Kwagilwa, amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika kuhakikisha rasilimali za ziwa hilo zinalindwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi na kukuza uchumi endelevu wa buluu.
Akizungumza katika Mkutano wa Maandalizi wa Mkutano wa 14 wa Mawaziri wa Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika unaofanyika Dar es Salaam, Kwagilwa alisema ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kulinda ikolojia ya ziwa hilo na kuhakikisha rasilimali zake zinaendelea kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisema Ziwa Tanganyika lina utajiri mkubwa wa viumbe hai na rasilimali za asili, huku takribani wakazi milioni 13 wakitegemea bonde hilo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na maisha yao ya kila siku.
Amesisitiza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi wanachama pamoja na wadau wengine kuhakikisha mkataba wa usimamizi endelevu wa ziwa hilo unatekelezwa kwa vitendo ili kuimarisha uhifadhi na kukuza uchumi unaotegemea rasilimali za ziwa.
“Tuko tayari kushirikiana na nchi wanachama na wadau wote ili kulinda ikolojia ya ziwa letu na kukuza uchumi endelevu wa buluu,” amesema Kwagilwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Kijani na Mazingira wa Jqmuhuri ya Zambia, Douty Chibamba, amezitaka nchi wanachama kuhakikisha maamuzi kuhusu usimamizi wa ziwa hilo yanaongozwa na ushahidi wa kisayansi, uwezekano wa kiufundi na ulinzi wa mazingira.
Amesema msisitizo huo ni muhimu hasa katika kushughulikia hatari za mafuriko na mabadiliko ya viwango vya maji ya ziwa, akieleza kuwa mapendekezo yoyote ya kuingilia mfumo wa ziwa yanapaswa kuzingatia athari zake kwa jamii na mazingira.
Chibamba ametaja mapendekezo ya uchimbaji wa Mto Lukuga na uwezekano wa kujenga bwawa la kudhibiti viwango vya maji kuwa miongoni mwa masuala yanayohitaji kuchambuliwa kwa kina kabla ya maamuzi kufikiwa.
Amesema hatua hizo zinaweza kuwa na athari kwa jamii, miundombinu, mifumo ya ikolojia na shughuli za kiuchumi zinazofanyika ndani ya bonde hilo, hivyo ni muhimu kufanya tathmini zinazozingatia ushahidi wa kisayansi.
Ameeleza kuwa mkutano wa maandalizi ni fursa kwa mawaziri, maofisa wakuu na wataalamu kutoka nchi wanachama kupitia nyaraka muhimu zitakazowasilishwa katika Mkutano wa 14 wa Mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa.
Amezitaja nyaraka hizo kuwa ni pamoja na mpango kazi na bajeti inayopendekezwa kwa mwaka 2027, ripoti ya mwaka ya Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika na nyaraka nyingine za kimkakati na kiufundi.
Katika eneo la uvuvi, Chibamba amesisitiza umuhimu wa kutumia matokeo ya tathmini za kisayansi za samaki kuongoza maamuzi kuhusu uhifadhi, uvunaji endelevu na ulinzi wa maisha ya wananchi wanaotegemea rasilimali hiyo.
Amezitaka nchi wanachama kuhakikisha mpango kazi na bajeti vinazingatia vipaumbele vya usimamizi endelevu wa ziwa, huku akihimiza kuimarishwa kwa utawala, uwajibikaji, uratibu na upatikanaji wa rasilimali za kifedha na watu ili kuboresha utendaji wa mamlaka hiyo.
Mkutano huo unawakutanisha wawakilishi wa Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Tanzania na Zambia kwa ajili ya kupitia masuala ya kiutendaji, kifedha, kimazingira na kiufundi yatakayowasilishwa katika Mkutano wa 14 wa Mawaziri wa Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika.

