
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Balozi Modest Jonathan Mero, akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere

Mlau wa Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Elizabeth Lulu Genda akitoa nasaha kwa wahitimu wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam yaliyofanyika tarehe 29 Oktoba 2026, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam

………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, wametakiwa kuwa waadilifu, wenye nidhamu na uwajibikaji, pamoja na kutoa huduma bora katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 25 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohamed Shein, amewapongeza wahitimu kwa juhudi, nidhamu na uvumilivu waliouonesha katika safari yao ya kitaaluma.
Dkt. Shein amesema mahafali hayo ni fursa ya kutambua mafanikio ya chuo katika kuimarisha ubora wa elimu, kukuza ubunifu na kupanua fursa za elimu ya juu. Amesisitiza kuwa wahitimu wana wajibu wa kutumia maarifa waliyoyapata kwa manufaa ya jamii.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema chuo hicho kinaendelea kuboresha programu za masomo ili ziendane na mahitaji ya soko la ajira na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.
Aidha, chuo kinaendelea kutumia utaalamu wa watumishi wake kutoa mafunzo na huduma za ushauri wa kitaalamu zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali.
Prof. Mwegoha amesisitiza umuhimu wa wahitimu kuendelea kujifunza, kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo Akili Mnemba (AI), pamoja na kutumia elimu yao kuwanufaisha wengine ili kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Balozi Modest Jonathan Mero, amewataka wahitimu kuzingatia nidhamu na kutumia elimu waliyoipata ipasavyo, wanapoajiriwa au kujiajiri, huku wakitengeneza fursa za ajira kwa wengine.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Mhitimu Bora wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, kwa mwaka 2026, Enoishi Kimirei, amewashukuru viongozi wa chuo, wahadhiri, watumishi, wazazi na walezi kwa mchango wao katika kufanikisha safari yao ya kitaaluma.
Mahafali hayo yamewakutanisha viongozi wa Chuo, wanataaluma, wahitimu, wazazi, walezi na wageni waalikwa kusherehekea mafanikio ya wahitimu wa mwaka wa masomo 2025/2026.
