Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

WANANCHI wa Miswe kata ya Mbwawa, Mailmoja ,Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, wamenufaika na huduma za msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Samia Legal Aid Awamu ya Pili, kuhusu haki za wananchi, masuala ya ndoa na familia, matunzo ya watoto pamoja na ukatili wa kijinsia.

Huduma hizo zimetolewa oktoba 29,2026 ambapo wananchi wamepata fursa ya kuwasilisha changamoto zinazowakabili na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria, huku watoa huduma wakikutana na Baraza la Usuluhishi wa Masuala ya Ndoa la kata kwa ajili ya kujadili changamoto za ndoa na familia.

Akizungumzia masuala ya ndoa, Mkurugenzi wa Kibaha Paralegal Centre, Catherine Mlenga, amewataka vijana na watu wanaotarajia kufunga ndoa kufikiria kwa kina kabla ya kufanya uamuzi huo, akieleza kuwa migogoro ya kifamilia na kuvunjika kwa ndoa vinaweza kuathiri malezi ya watoto na kuchangia baadhi yao kuishi mitaani.

Mlenga amesema kituo hicho kimekuwa kikipokea changamoto nyingi zinazohusu ndoa na familia, zikiwemo migogoro ya talaka, kutelekezwa kwa watoto, migogoro ya mirathi na wanawake kunyimwa haki zao, hali inayodhihirisha umuhimu wa wananchi kupata elimu ya kisheria ili waweze kutambua na kudai haki zao kwa njia zinazostahili.

Ameeleza kuwa, pamoja na kutoa msaada wa kisheria na kusaidia usuluhishi wa migogoro katika jamii, kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha za kuendesha shughuli zake, hivyo kuiomba Serikali kutimiza ahadi za kutoa fedha na ofisi kwa vituo vya msaada wa kisheria ili viweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Sambamba na huduma hizo kwa wananchi, timu ya watoa huduma wa Samia Legal Aid imetembelea Shule ya Sekondari Mbwawa na Shule ya Msingi Miswe, ambako wanafunzi wamepatiwa elimu kuhusu kujitambua, kufahamu haki zao, kujikinga na ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kutoa taarifa kwa walimu, wazazi, walezi au mamlaka husika wanapokumbana na vitendo hivyo.