*Afungua Rasmi Maonesho ya 10 ya Madini, asisitiza Ushiriki wa Kampuni za Kizawa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, amefungua rasmi Maonesho ya 10 ya Madini yanayoendelea katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, huku akipongeza mchango wa wadau katika kukuza sekta ya madini nchini.
Katika hotuba yake, Eng. Samamba amezipongeza taasisi na wadau mbalimbali kwa juhudi wanazofanya katika kuendeleza sekta hiyo, akisisitiza kuwa ushiriki wao una mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta ya madini na uchumi wa Taifa.
Aidha, amepongeza uongozi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMISA) kwa juhudi unazoendelea kuchukua katika kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content), hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa kampuni za ndani na kunufaisha Watanzania kupitia rasilimali za madini.
Baada ya ufunguzi, Eng. Samamba alitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo, ambako alipata fursa ya kujionea vifaa, mashine na teknolojia mbalimbali zinazotumika katika shughuli za madini.
Pia, alifurahishwa na mwitikio wa kampuni za kizawa zilizoshiriki maonesho hayo, akiwapongeza wadau kwa kuonesha bidhaa, huduma na teknolojia zinazochangia maendeleo ya sekta ya madini

