
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi akishuhudia utiaji Saini leseni za utafutaji wa mafuta na gesi katika vitalu vya Mnazi bay north, West Songo songo, Eyasi wembere na Lindi – Mtwara, katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo Tarehe 28 Oktoba 2026. Anayesaini ni Waziri wa Nishati Dkt. Juma Homera.

Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, (kushoto) akisaini kitabu wakati alipotembelea banda la ETDCO leo, katika hafla ya utiaji Saini Leseni za Utafutaji wa Mafuta na Gesi katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi Wembere na Lindi-Mtwara, wa kwanza kulia ni Kaimu Naibu Meneja Mkuu wa Huduma za Ufundi wa ETDCO , Mhandisi Abdallah Mitenda


Afisa Uhusiano Kampuni ya ETDCO Samia Chande (kulia) akitoa elimu kwa wadau mbalimbali waliotembelea banda la Kampuni hiyo katika hafla ya utiaji Saini Leseni za Utafutaji wa Mafuta na Gesi katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi Wembere na Lindi-Mtwara


…….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Nishati kuhakikisha Watanzania wanapewa kipaumbele katika fursa za ajira, mafunzo, uhamishaji wa teknolojia na zabuni, huku kampuni za ndani zikiwezeshwa kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya nishati.
Akizungumza Oktoba 28, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utiaji saini leseni za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi Wembere na Lindi–Mtwara, iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Mhe. Ndejembi, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya tathmini, ufuatiliaji na usimamizi wa leseni hizo ili kuhakikisha utekelezaji wake unaleta manufaa kwa Taifa.
Akizungumzia ushiriki wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) katika hafla hiyo, Kaimu Naibu Meneja Mkuu wa Huduma za Ufundi wa kampuni hiyo, Mhandisi Abdallah Mitenda, amesema ETDCO inalenga kutumia fursa zinazotokana na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa kuomba na kupata miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo husika, hususan mikoa ya Lindi na Mtwara.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa dini na wadau wa sekta ya nishati, ETDCO ilitoa elimu kuhusu majukumu yake pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ya umeme, ikiwemo miradi ya usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Ushiriki huo ni sehemu ya juhudi za ETDCO za kuimarisha uhusiano na wadau wa sekta ya nishati, kutangaza uwezo wake wa kitaalamu na kujipanga kunufaika na fursa zinazotokana na uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini.
