Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amewataka Wanachuo katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi – Mbalizi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Hayo amezungumza Oktoba 28, 2026 katika muendelezo wa kampeni ya “Ongea na Kamanda” na “Ongea na Freshers” baada ya kutembelea na kuongea na Wanachuo wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Afya Mbalizi ambapo amekemea tabia ya uchochezi inayofanywa na baadhi ya Wanavyuo kupitia mitandao ya kijamii na kujikuta kwenye mikono ya Serikali.

“Niwatake kujiepusha na vitendo vya kuandaa na kusambaza taarifa za uchochezi dhidi ya Serikali na watu wengine kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na itawasababisha kupoteza malengo yenu na ndoto zenu za kimaisha” alisema Kamanda Kuzaga.

Naye, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Kaneng Muro amewataka Wanafunzi hao kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kupitia utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu mapema ili ziweze kufanyiwa kazi na kuleta matokeo chanya ikiwemo kukamatwa kwa watuhumiwa wa matukio ya uhalifu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa mtoto Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Veronica Ponera amewataka Wanafunzi hao kujiepusha na vitendo vya ukatili na unyanyasaji, amekemea ukatili wa kingono, kimwili na kisaikolojia kwani ni hatari kwa usalama wao.

Mkurugenzi wa Chuo hicho, Marcos Lenna amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kubuni programu hizo zenye lengo la kutoa elimu na kupata kusikia kero, changamoto na maoni kutoka kwa jamii kuhusiana na masuala ya ulinzi na usalama ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali.