Na Mwandishi Wetu, Pwani.

26 Oktoba 2026.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Kanda ya Mashariki, imebaini kuwa maduka 19 kati ya 38 ya dawa muhimu yaliyokaguliwa katika Wilaya ya Mafia hayakuwa na watoa huduma wenye sifa zinazotakiwa kisheria, sawa na asilimia 50.0 ya maduka yote ya dawa muhimu yaliyopo katika wilaya hiyo.

Hali hiyo inaweza kuhatarisha afya za wananchi iwapo wataendelea kupata huduma za dawa kutoka kwa watu wasio na sifa zinazotakiwa kisheria.

Hayo yamebainika kufuatia ukaguzi maalumu uliofanywa na TMDA wilayani humo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa muda wa siku 10, kuanzia tarehe 11 hadi 23 Oktoba 2026.

Ukaguzi huo ulilenga kuhakikisha kuwa maeneo yanayotoa huduma za dawa na vifaa tiba yanafanya shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayohusika.

Akizungumza wakati wa kutoa mrejesho wa ukaguzi huo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Mkaguzi Mwandamizi wa Dawa aliyeongoza timu ya ukaguzi, Bw. Japhari Saidi, alisema kuwa mbali na changamoto ya ukosefu wa watoa huduma wenye sifa zinazotakiwa kisheria, timu hiyo ilibaini ukiukwaji mwingine wa Sheria na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa maduka ya dawa muhimu.

Alisema kuwa maduka 10 yalikuwa yakifanya biashara bila vibali vinavyotakiwa, kinyume na kifungu cha 18 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, sawa na asilimia 26.3 ya maduka 38 yaliyokaguliwa.

Aidha, maduka 13 yalikuwa yakiuza dawa ambazo haziruhusiwi kuuzwa katika maduka ya dawa muhimu, kinyume na Kanuni za Makundi ya Dawa, sawa na asilimia 34.2. Vilevile, maduka sita (6) yalikutwa yakiuza dawa zisizosajiliwa kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria hiyo, sawa na asilimia 15.8.

Katika hatua nyingine, maduka matatu yalibainika kutoa huduma za kitabibu, ikiwemo kufanya vipimo vya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), kinyume na matakwa ya Sheria, sawa na asilimia 7.9 ya maduka yaliyokaguliwa.

Kufuatia kubainika kwa ukiukwaji huo, TMDA ilichukua hatua mbalimbali za kiudhibiti kwa mujibu wa Sheria, ikiwemo kuondoa dawa ambazo hazikustahili kuuzwa katika maduka hayo na kuwaelekeza wamiliki wa maduka yasiyokuwa na watoa huduma wenye sifa kusitisha huduma hadi yatakapopata watoa huduma wanaokidhi matakwa ya kisheria.

Aidha, faini za papo kwa papo zilitozwa kwa makosa yaliyostahili hatua hiyo, ambapo jumla ya shilingi milioni 2.9 zilitozwa. Kufikia tarehe 25 Oktoba 2026, faini zote zilizotozwa zilikuwa zimelipwa.

Kwa upande wake, Mfamasia wa Wilaya ya Mafia, Bw. Kurwa Lucas, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya TMDA na Halmashauri hiyo na kuahidi kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwa kila duka ili kuhakikisha kuwa wahusika wanazingatia matakwa ya kisheria.

Hatua hizo zinalenga kuhakikisha kuwa wananchi wa Mafia wanapata huduma za dawa zinazokidhi viwango vinavyotakiwa na kulindwa dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya dawa zisizosajiliwa, uuzaji wa dawa zisizoruhusiwa na utoaji wa huduma na watu wasio na sifa zinazotakiwa kisheria.