Na Sophia Kingimali

MFUKO wa Taifa wa huduma ndogo za kifedha (Self Microfinance Fund SELF MF) umefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 138 katika kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka 2023 hadi 2026, na kuwafikia wanufaika 131,312, hatua iliyochochea shughuli za kiuchumi na kutengeneza ajira 262,624 nchini.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya mfuko huo leo Octoba 28,2026 Jijini Dar es salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Self Microfinance Fund Santieli Yona amesema mafanikio hayo yanaonesha mchango wa taasisi hiyo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia upatikanaji wa huduma za kifedha na mikopo inayolenga makundi mbalimbali ya jamii.

Amesema katika kipindi hicho, mfuko umeweza kupata faida ya Sh bilioni 3.19, jambo linaloonesha uwezo wake wa kuendesha shughuli zake kwa ufanisi na kutumia vizuri mtaji uliowekezwa na Serikali, huku ukiendelea kutoa huduma kwa wananchi wanaohitaji mitaji kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara zao.

Ameongeza kuwa mafanikio mengine ni kutoa gawio la Sh milioni 490 kwa Serikali katika kipindi cha miaka mitatu, hatua inayochangia mapato ya Serikali na kuonesha kuwa taasisi hiyo ina uwezo wa kujiendesha kibiashara huku ikitekeleza jukumu lake la kijamii la kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Aidha Yona amesema,mfuko umeendelea kutoa mikopo ya aina mbalimbali kwa wajasiriamali wadogo, wakulima, wafugaji, wavuvi na makundi mengine ya wananchi, pamoja na kuwezesha taasisi za kifedha kama SACCOS na AMCOS kupata fedha za kukopesha wanachama wao, ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mitaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kupitia mikopo hiyo, baadhi ya wanufaika wameweza kupanua shughuli zao za biashara na kuongeza uwezo wa kiuchumi, akieleza kuwa kuna wateja walioanza na mikopo midogo na baadaye kufikia uwezo wa kukopa kiasi kikubwa zaidi. 

Amesema mfuko huo pia unatoa mikopo ya maendeleo ya makazi inayowawezesha wananchi kukamilisha nyumba zao, pamoja na mikopo kwa watumishi wa umma, huku ukiendelea kubuni bidhaa zinazolenga kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali na kuongeza fursa za kujikwamua kiuchumi.

Katika kuunga mkono ajira na uwezeshaji wa vijana, amesema Self imeweka bidhaa za mikopo zinazowawezesha vijana kumiliki vyombo vya usafiri, ikiwemo bajaji, kwa ajili ya kujiajiri na kujipatia kipato. Hatua hiyo inalenga kuongeza fursa za ajira na kuwasaidia vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya taifa.

Ameeleza kuwa mafanikio mengine ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia mtandao wa matawi 12 na vituo viwili vya huduma vilivyofunguliwa mikoa ya Kigoma na Katavi, huku taasisi hiyo ikiendelea kutoa huduma katika mikoa mbalimbali kwa kutumia mfumo wa matawi yanayohudumia maeneo zaidi ya mkoa mmoja.

Amesema katika mpango wa miaka mitano ijayo, mfuko unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma kwa njia za kidijitali ili wananchi waweze kupata taarifa na huduma za mikopo kwa urahisi zaidi bila kulazimika kufika katika matawi yake, hatua inayotarajiwa kupunguza changamoto za umbali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Amebainisha kuwa Self pia imejikita katika kukuza matumizi ya nishati safi kwa kutoa mikopo inayowawezesha wananchi kupata majiko yanayotumia umeme kwa kiwango kidogo, pamoja na bidhaa nyingine zinazolenga kulinda mazingira. Amesema hatua hiyo inaendana na juhudi za taifa za kuhifadhi mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika shughuli za kila siku.

Aidha, amesema mfuko umeendelea kutoa elimu ya fedha kwa wanufaika kabla na baada ya kupata mikopo ili kuwasaidia kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, kupanga marejesho na kuendesha biashara kwa ufanisi. Ameeleza kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kuongeza uelewa wa gharama za mikopo na kuimarisha utamaduni wa kurejesha fedha kwa wakati.

Amesema pamoja na mafanikio hayo, mfuko unakabiliwa na changamoto za uelewa mdogo wa elimu ya fedha kwa baadhi ya wananchi, kutokuwepo kwa utamaduni wa kurejesha mikopo kwa wakati na biashara nyingi za wajasiriamali wadogo kutokuwa rasmi. Hata hivyo, taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu, kuhamasisha urasimishaji wa biashara na kuwashauri wateja kufuata taratibu zinazohitajika ili kuongeza nafasi zao za kupata huduma za kifedha.

Amesisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana yanatoa msingi wa kuendeleza juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuongeza ajira na kukuza biashara, huku mfuko ukiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kufikisha huduma kwa wananchi wengi zaidi. Amesema lengo ni kuhakikisha mikopo inakuwa nyenzo ya kuongeza kipato cha wanufaika, kukuza uchumi jumuishi na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.