📍 DODOMA
Wahariri, wasanii, wanafunzi wa vyuo vikuu na watengenezaji wa maudhui ya mitandaoni wamefanya ziara katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kuelekea uzinduzi wa majengo na miundombinu yake utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Oktoba 30, 2026.
Akizungumza Oktoba 28,2026 baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema uzuri na mpangilio wa mji huo ni somo linaloweza kutumiwa katika kuboresha maeneo mengine ya nchi, ikiwemo Dar es Salaam. Ameipongeza Serikali, wahandisi na viongozi waliohusika katika utekelezaji wa mradi huo, akitaja marais wa awamu zilizoshiriki kuanzia Dkt. John Magufuli hadi Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wao, wasanii walioshiriki ziara hiyo wameeleza kushangazwa na ukubwa na ubora wa majengo pamoja na miundombinu iliyopo, wakisema mradi huo ni fursa kwa wasanii, jamii na taifa kwa ujumla. Wamesema kukamilika kwa mji huo kunaonesha hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa azma ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya shughuli za Serikali.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema mji huo umejengwa kwa kuzingatia mifumo ya kisasa ya utoaji huduma, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika kurahisisha shughuli za Serikali. Amesema uwekezaji huo umeifanya Mtumba kuwa mji wa kisasa unaoweza kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, huku wananchi wanaoweza kutumia mifumo ya Serikali Mtandao wakihudumiwa bila kulazimika kufika katika ofisi husika.

Aidha, amesema Kuwa Serikali imejenga kilomita 59 za barabara za lami ndani ya Mji wa Serikali Mtumba ili kurahisisha usafiri na ufikikaji wa ofisi mbalimbali. Ameongeza kuwa mji huo pia umeanza kuwa kivutio cha utalii jijini Dodoma, ambapo wageni wanaotembelea jiji hilo wanaweza kujifunza kuhusu mpangilio wa majengo, miundombinu na mifumo ya kisasa iliyowekwa kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma za Serikali.
