Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, Mhe. Vita Rashid Kawawa, amewataka viongozi na watendaji wa wilaya hiyo kuwasikiliza wananchi, kushughulikia malalamiko yao na kutatua kero zinazowakabili kwa wakati, ili kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali na kuongeza uelewa kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mhe. Kawawa ametoa agizo hilo leo tarehe Oktoba 28, 2026 wakati akifungua mafunzo ya Uraia na Utawala Bora kwa viongozi na watendaji katika Wilaya ya Hanang’, akisisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi kuhakikisha wananchi wanasikilizwa, wanapewa majibu ya hoja zao na kupata ufumbuzi wa changamoto wanazowasilisha katika maeneo yao.
Amesema kuwa usikilizaji wa wananchi na utatuzi wa changamoto zao ni miongoni mwa misingi muhimu ya utawala bora, inayosaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya Serikali na wananchi huku akiwataka viongozi kuwaeleza wananchi kuhusu kazi na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ili kuongeza uelewa, ushiriki na imani yao katika shughuli za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Kawawa amesisitiza umuhimu wa viongozi na watendaji kutoa kipaumbele kwa makundi yenye uhitaji maalumu, yakiwemo watu wenye ulemavu, wajane na wagane, kwa kuhakikisha wanapata huduma stahiki na kutendewa haki bila ubaguzi na kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa huduma.
Awali Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Katiba Idara ya Katiba na Ufuatiliaji wa Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Prosper Kisinini, amewataka viongozi na watendaji kutokata tamaa katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakizingatia misingi ya haki, uwajibikaji na utawala bora.
Kisinini amesisitiza kuwa watendaji wanapaswa kutenganisha migogoro binafsi na majukumu yao ya kikazi, pamoja na kuhakikisha kuwa maamuzi wanayoyafanya yanazingatia sheria, haki na usawa bila upendeleo wala kumuonea mtu yeyote.
Mafunzo hayo ni jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria katika kuwajengea viongozi na watendaji uelewa wa misingi ya uraia na utawala bora, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuchangia utoaji wa huduma bora kwa wananchi ili kufika Dira ya Maendeleo 2050.

