Na Silivia Amandius
Bukoba.
Wajasiriamali zaidi ya 50 wanaojishughulisha na biashara ya senene katika Manispaa ya Bukoba wanatarajia kunufaika na maboresho ya soko lao jipya lililopo Kata ya Bilele, katika Uwanja wa Mayunga, maarufu Uswahilini, kufuatia msaada waliopatiwa na Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Samira Khalfan Amour.
Msaada huo umetolewa kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali hao kuimarisha mazingira ya biashara zao na kuendelea kujipatia kipato kupitia biashara ya senene, ambapo sehemu kubwa ya wafanyabiashara hao ni wanawake. Miongoni mwa mahitaji yaliyofanyiwa kazi ni rangi ya kupaka soko, silingibodi za kufunika sehemu za ndani ya soko pamoja na kulipia gharama zote za kuunganisha umeme.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Mhe. Samira Oktoba 27, 2026, Katibu wake, Edina Makoye, amesema mbunge huyo ameguswa na juhudi zinazofanywa na wajasiriamali hao na kuamua kuwasaidia ili waweze kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Amesema Mhe. Samira anatambua umuhimu wa biashara hiyo katika maisha ya wajasiriamali hao, hivyo ameamua kuchangia mahitaji hayo ili kuboresha soko lao jipya. Aidha, amewahakikishia kuwa mbunge huyo ana nia ya kuwatembelea baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge ili kuwasalimia na kufahamu maendeleo yao.
Kwa upande wao, wajasiriamali hao wamemshukuru Mhe. Samira kwa kuitikia ombi lao kwa haraka, wakieleza kuwa msaada huo umewapa faraja wakati walipokuwa wakikabiliwa na changamoto za kifedha katika kukamilisha mahitaji ya soko lao.
Wamesema kitendo hicho kimeonesha upendo na kujali kwa mbunge huyo, licha ya kutokuwa mkazi wa Manispaa ya Bukoba, na kuongeza kuwa msaada huo utachangia kuboresha mazingira yao ya kufanyia biashara.
Msaada huo umekuja siku chache baada ya wajasiriamali hao kutoa wito kwa wadau wa biashara ya senene kujitokeza kuwasaidia kukamilisha soko lao jipya, baada ya kueleza kuwa gharama za ujenzi na mahitaji mengine zimekuwa mzigo mkubwa kwao.
Awali, wafanyabiashara hao walikuwa wakifanya shughuli zao katika eneo la Kanoni Darajani, lakini walihamishwa kutokana na eneo hilo kutokuwa rasmi kwa sababu ya kuwa ndani ya hifadhi ya barabara. Hali hiyo iliwalazimu kutafuta eneo jipya la kuendeleza biashara yao, hatua iliyoibua changamoto za gharama za kuandaa soko hilo.

