Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Nkoba Mabula ameupongeza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa uboreshaji wa miundombinu ya barabara, maji, umeme, mawasiliano, vitendea kazi pamoja na utoaji elimu kwa watumishi na wadau mbalimbali kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na Mvua za El-nino zinazotarajiwa 

Akiwa katika ukaguzi wa miundombinu Ngorongoro Mabula ameelekeza spidi kuongezeka kuboresha miundombinu ya maeneo hatarishi, mitambo, huduma za afya na kutoa Mafunzo ya vitendo kwa timu za uokoaji zinazohusisha maafisa na Askari wa jeshi la uhifadhi 

“Kama Elnino itakuja itukute tumeshajiandaa, mitambo, magari ya huduma, mafuta, na vipuri viwepo mda wote ili kuhakikisha usalama wa watalii, wananchi na rasilimali za Wanyamapori na malikale zilizopo pamoja na kuweka alama kwenye maeneo ambayo ni hatarishi ili kuongeza tahadhari kwa watumiaji” aliongeza Mabula. 

Akizungumza kwa Niaba ya Kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro, SACC Gloria Bideberi ameeleza kuwa katika kukabiliana na janga hilo hadi sasa imetoa

elimu kwa Watumishi 200, Viongozi wa Vijiji na Kata 275, wanafunzi wa shule zaidi ya 1550, Wananchi 4,965 kwenye kata 10 zilizopo ndani ya hifadhi,maeneo ya huduma za malazi 80 na kuandaa magari ya magonjwa matatu na vifaa tiba.

Mratibu wa shughuli za Miundombinu Eng. Shaban Felician amebainisha kuwa mitambo zaidi 11 imeandaliwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara na uokozi wa magari ya wageni sambamba na kuhakikisha mtandao wa barabara ndani ya hifadhi wenye zaidi ya kilomita 600 zinapitika katika msimu wote wa mvua.