Na John Walter -Babati
Katika kuadhimisha miaka 20 ya Polisi Jamii nchini Tanzania, Makala hii inaangazia namna gani Polisi Jamii imewaunganisha Polisi na Wananchi Mkoani Manyara na kufanikisha kubaini na kuzuia uhalifu mkoani hapa.
Katika kuzungumzia hilo, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Kija Mkoyi amesema Mkoa huu unaendelea kutambua umuhimu wa ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kudumisha amani, usalama na kupambana na uhalifu kupitia dhana ya Ulinzi Shirikishi.
Kupitia dhana hii, ACP Kija anasema, wananchi mkoani hapa wameendelea kuhamasishwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu, kushiriki katika kutatua changamoto za kiusalama na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na madhara ya kujihusisha na uhalifu.
Aidha, ushirikiano huu umeimarisha mawasiliano na kujenga uaminifu kati ya Polisi na wananchi mkoani hapa huku ukichochea dhana ya usalama kuwa jukumu la kila mmoja katika jamii kuanzia ngazi ya familia, Mtaa, Kijiji mpaka kitongoji.
Vile vile, amesema katika Mkoa wa Manyara, wananchi wanahimizwa kuendeleza ushirikiano na Polisi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za ulinzi na usalama katika maeneo yao.
“Polisi Jamii ni msingi wa usalama shirikishi, tushirikiane kulinda maisha, mali na amani kwa maendeleo ya Mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla” anasema ACP Mkoyi
Ikumbukwe kuwa Dhana na Falsafa ya Polisi Jamii nchini Tanzania ilianzishwa rasmi mwaka 2006 na mpaka sasa ina jumla ya miradi 23 ya Polisi Jamii inayotekwlezwa, miongoni mwa miradi hiyo ni Mradi wa Polisi Kata, Usalama wetu kwanza, uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi, kupinga ukatili wa kijinsia, kupinga matumizi ya dawa za kulevya, muongo rika, mazingira salama, uvuvi salama, mazizi salama na miradi mingine 15 inayotekeleza na Polisi nchi nzima.
Kuanzishwa, kusimamiwa na kutekelezwa kwa falsafa ya Polisi Jamii nchini kumeleta matokeo chanya katika dhana ya kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kwani jamii imepata elimu na kuwa tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu na kushiriki ulinzi kupitia vikundi vya ulinzi shirikishi.
