Na Mwandishi Wetu– Dar es Salaam
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetumia Sh bilioni 12.9 kununua mashine za kisasa za maabara, huku likitoa vyeti na leseni 3,940 za ubora kwa wazalishaji, wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683, katika juhudi za kuimarisha ubora na usalama wa bidhaa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura A. Katunzi, ameeleza hayo katika wasilisho la shirika hilo wakati wa kikaokazi cha wahariri wa vyombo vya habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kufanyika katika ofisi za TBS, Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Katunzi amesema uwekezaji huo unaenda sambamba na kuimarisha miundombinu ya maabara na ofisi za kanda ili kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza ufanisi wa upimaji wa sampuli na kuhakikisha bidhaa zinazouzwa nchini zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
Amesema TBS ina maabara 14 ambazo zote zimepata ithibati za umahiri wa kimataifa, huku katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita maabara hizo zikipima sampuli zaidi ya 188,952 na kufanya ugezi wa vifaa 54,396.
Baadhi ya mashine za kisasa zilizopo katika maabara hizo ni kifaa cha kupima mabomba ya maji kwa shinikizo, mashine ya kupima ukinzani wa nyaya za umeme na mashine ya kupima paneli za sola bila kutegemea uwepo wa jua.
Katika kuimarisha upatikanaji wa huduma, Dkt. Katunzi amesema Serikali imetumia zaidi ya Sh bilioni 9.8 kuboresha ofisi tisa za kanda pamoja na ofisi za mipakani, bandarini na viwanja vya ndege kwa kuongeza wafanyakazi na vitendea kazi.
Aidha, mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara wa Viwango House Mwanza unakadiriwa kugharimu Sh bilioni 12.1, huku maandalizi ya awali ya mradi kama huo yakianza jijini Arusha.
Amesema maabara za Dodoma zinahudumia pia mikoa ya Singida na Tabora, wakati maabara za Mwanza zinatarajiwa kuhudumia mikoa sita ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
Katika kuwezesha biashara, Dkt. Katunzi amesema shirika limeandaa viwango 3,901 katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kupitia kamati zake 117 za kitaalamu, zinazoshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wazalishaji, wafanyabiashara, vyuo vikuu na taasisi za utafiti.
Amesema viwango hivyo vinasaidia wazalishaji na wajasiriamali kutengeneza bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko na kuongeza uwezo wao wa kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa Serikali hutenga zaidi ya Sh milioni 300 kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali wadogo katika kupata vyeti na leseni za ubora bila malipo, hatua inayolenga kuwawezesha kuboresha bidhaa zao na kupanua masoko.
Katika usajili na ukaguzi wa bidhaa, TBS imesajili bidhaa 9,731 za chakula na vipodozi pamoja na maeneo 80,836 yanayohusika na uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa bidhaa hizo.
Vilevile, shirika limekagua shehena za bidhaa 183,186 kabla ya kusafirishwa kuja nchini kupitia mfumo wa Pre-Shipment Verification of Conformity (PVoC), huku shehena nyingine 426,842 zikikaguliwa baada ya kuwasili nchini kupitia mfumo wa Destination Inspection (DI). Magari 249,386 yaliyotumika nayo yalikaguliwa.
Ukaguzi huo unalenga kuzuia bidhaa zisizokidhi viwango kuingia sokoni na kulinda afya, usalama na mazingira ya watumiaji.
Katika kujenga uwezo wa wazalishaji, TBS imetoa mafunzo kwa wadau 6,824 kuhusu viwango na udhibiti wa ubora. Shirika pia linaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia kliniki za viwango, maonesho, semina, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Kwa upande wa matumizi ya teknolojia, Dkt. Katunzi amesema TBS imeimarisha mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za leseni za ubora, ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi. Mfumo wa Online Application System (OAS) umeunganishwa na mfumo wa Dirisha Moja la Huduma za Serikali za Kielektroniki Tanzania (TeSWS) ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wafanyabiashara.
Amesema shirika pia limeshirikiana na Wizara ya Nishati na wadau wa maendeleo kuanza kuandaa viwango vya ufanisi wa nishati kwa vifaa vya umeme vya majumbani, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Mafanikio ya TBS yameambatana na tuzo na ithibati mbalimbali za kitaifa na kimataifa, ikiwemo kutambuliwa kama Taasisi Bora ya Udhibiti Barani Afrika mwaka 2023 na kupata ithibati katika mifumo ya usimamizi wa ubora na ukaguzi.
Dkt. Katunzi amesema shirika litaendelea kuimarisha huduma zake kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali ili kuwezesha biashara, kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama.
Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za TBS za kuimarisha udhibiti wa viwango na kuboresha huduma kwa umma.

