Na Sixmund Begashe, Arusha
WIZARA ya Maliasili na Utalii inazidi kujiimarisha katika nyanja ya Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) wa utekelezaji wa majukumu yake na taasisi zilizo chini yake kwa kuanza kuandaa mfumo utakaotumika kuongeza kasi kwenye nyanja hiyo muhimu ujulikanao kama ‘M&E Framework’.
Akizungumza na wataalam wa M&E wa Wizara hiyo na taasisi zake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Nkoba Mabula, amesema Wizara ina matumaini makubwa na wataalam hao hivyo wakitumie vyema Kikao Kazi hicho katika kuipeleka Wizara kwenye hatua muhimu ya matumizi ya ‘M&E Framework’.
Bw. Mabula amezipongeza idara, vitengo na taasisi za Wizara hiyo kwa kushiriki kwenye Kikao Kazi hicho kinachofanyika katika Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara, Arusha, kwa kuwa matokeo yake yatasaidia kuchechemua zaidi utendaji wa shughuli za Wizara hiyo.
Akizungumza katika Kikao Kazi hicho, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Bure Nassibu, amesema lengo la kuwakutanisha wataalam wa Wizara na taasisi zake ni kuimarisha uelewa wa pamoja juu ya maandalizi na matumizi ya mfumo huo kwa njia shirikishi.
Ameongeza kuwa, maandalizi ya mfumo huo, yatajengwa na msingi wa uwezeshwaji utakaofanywa na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Taasisi ya Uongozi na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu ambapo washiriki hao watapitia mipango ya kitaifa ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Muda Mrefu (LTTP, 2026/2027 – 2050/2051), Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, (2026/2027 – 2030/2031) pamoja na Mpango Mkakati wa Wizara (2026/2027 – 20230/2031).
Akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Bw. Bernard Marcelline, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Bi. Eunice Msangi na maafisa wengine, Bw. Mabula yuko katika ziara ya kikazi jijini Arusha kwa ajili ya kukagua miundombinu ya hifadhi hiyo ikiwa ni maandalizi ya Wizara kujikinga na athari za mvua za El Nino zinazotabiriwa kujitokeza na kuathiri maeneo ya hifadhi na utalii.

