Singida. 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego amezindua mpango wa matengenezo ya kawaida ya barabara kwa kutumia vikundi vya kijamii (CBRM) na kukabidhi mikataba na vitendea kazi kwa vikundi 41 vitakavyotekeleza mpango huo mkoani humo. 

Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 26, 2026 katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa huo pamoja na wawakilishi wa vikundi 41 vya kijamii vinavyotokana na makundi ya Vijana, akina Mama, Wazee na watu wenye ulemavu.

Akizungumzia katika hafla hiyo Mhe. Dendego amesema Serikali ya Tanzania imeutangazia ulimwengu inaenda kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050 na imeweka malengo mahsusi ikiwa ni pamoja na kutaka kuwa na uchumi wa kati ambao ni jumuishi, endelevu na stahamilivu. 

Amesema unaposema uchumi lazima uwaguse watu na kuongeza kuwa ili uchumi huo uwe endelevu na jumuishi lazima uguse yale makundi maalum katika jamii. 

“Kwa hiyo sisi kupitia programu hii ya TARURA tumeanza kutekeleza Dira kwa vitendo ndio maana nampongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Sera na Mipango inayotekelezeka na sisi wasaidizi wake kazi yetu ni kupokea na kutekeleza na leo tumeianza safari hii kupitia TARURA”. Amesema Mhe. Dendego.

Mhe. Dendego amebainisha kuwa hapo awali kazi hizo zilikuwa zinafanywa na Wakandarasi wakubwa ambao walikuwa hawatoki mkoani humo lakini leo hela ya Singida inaletwa Singida na kuwanufaisha wananchi wa Singida na kuongeza kuwa hayo sio tu mabadiliko makubwa ya kiuchumi lakini inaonesha dhamira ya dhati ya serikali kuhakikisha kila mkoa lazima watu wake wanaendelea kiuchumi kupitia programu mbalimbali ikiwemo hii ya CBRM.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Claver Mwinuka amesema Mpango wa CBRM Mkoa wa Singida umetengewa jumla ya shilingi milioni 889 ambazo zimegawanywa katika wilaya tatu ambazo ni Wilaya ya Mkarama shilingi milioni 122, Ilamba shilingi milioni 383, Halmashauri ya Manispaa ya Singida na Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini shilingi milioni192 kwa kila Halmashauri. 

Mhandisi Mwinuka amefafanua kuwa katika awamu hii mpango huo wa CBRM unaenda kuzihudumia barabara zenye urefu wa km 232 kutoka halmashauri nne za Wilaya tatu ambazo zimetoa jumla ya vikundi 41vitakavyotekeleza kazi hizo za matengenezo ya kawaida ya barabara katika halmashauri zao. 

Akielezea manufaa ya mpango huo Kwa TARURA na Vikundi hivyo, Mhandisi Mwinuka amesema hapo awali walikuwa wakiwatumia wakandarasi wakubwa kutekeleza jukumu hilo hususani kufyeka nyasi pembezoni mwa barabara lakini walijikuta yale malengo ya matengenezo kwa maana ya kufyeka nyasi na shughuli nyingine za matengenezo ili barabara ziweze kuonekana vizuri hivyo kuepusha ajali za barabarani yalikuwa hayajafikiwa.

Mhandisi Mwinuka amesema kwa sasa kupitia vikundi hivyo wanaenda kupata usaidizi kwa maana ya utunzaji wa barabara unaenda kuimarika lakini pia vikundi hivyo vitaimarika kiuchumi wao wenyewe na kwa sababu vikundi hivyo vimesajiliwa kwenye mfumo wa manunuzi wa NEST vikundi hivyo vinaweza kupata kazi katika taasisi nyingine za umma.

Kwa upande wao wawakilishi wa vikundi hivyo ambao ni Bw. Ibrahim Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi cha Vijana cha Jitume Group na Bi. Rose Mbelwa Katibu wa kikundi cha akina mama cha J. THELL Women wameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kupata fursa hiyo na wamejipanga kufanya kazi kwa bidii, weledi na kujituma hivyo kupelekea wao wanavikundi kuinua vipato vyao na kuweza kuzihudumia familia zao vizuri.