Na Mwandishi wetu, Mirerani

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamelalamikia kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kitendo cha migodi mingi ya madini ya Tanzanite kutochangia miradi ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na tozo za huduma kwa jamii.

Madiwani wa Halmashauri hiyo wametoa kilio hicho kwa kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Subira Mgalu ilipofanya ziara katika machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kaleiya Melita Mollel amesema wamiliki wengi wa madini ya Tanzanite hawachangii maendeleo kupitia CSR au ushuru wa huduma.

“Ni kampuni chache ambazo zinafanya CSR au kutoa service levy jambo ambalo lipo kisheria lakini wamekuwa wazito ila kampuni za Franone, Chusa Mining, God Charity na bilionea Laizer wamekuwa wanashiriki,” amesema.

Mwenyekiti wa kamati ya Elimu, Afya na Maji kwenye Halmashauri hiyo, Albert Msole amesema suala la kuchangia fedha kwenye Halmashauri hiyo lipo kisheria ila kampuni za uchimbaji hazina mwitikio wa kuchangia.

Msole amesema halmashauri hiyo inabeba mzigo wa kulea na kusomesha baadhi ya watoto yatima ambao wazazi wao walifariki dunia kwa kuugua vifua migodini.

“Suala la makampuni ya uchimbaji kuchangia CSR limekuwa kama hisani japokuwa lipo kisheria, ni makampuni machache yaliyotajwa na Mwenyekiti ndiyo yanachangia CSR,” amesema Msole.

Naibu Waziri wa Madini, Steven Lemomo Kiruswa amesema suala la kuchangia CSR linapaswa kutiliwa maanani na makampuni ya uchimbaji kwani yapo kisheria.

“Hata kule Geita ambapo CSR inafanya vyema, bado wabunge wa kule wanalalamikia kiwango kinachotolewa ni kidogo hivyo kinapaswa kiongezwe,” amesema Dkt Kiruswa.

Kamishna wa Madini Dkt Abdurahman Mwanga amesema suala la CSR ni lazima kwani lipo kisheria kifungu cha 105 na halmashauri zinapaswa ziweke muongozo wa namna ya kuchangia.

“Kuhusu suala la service levy inapaswa kuchangia asilimia 00.3 ya mauzo ghafi kwa mwaka nayo inapaswa kuchangiwa na kampuni zilizopo hapa Simanjiro,” amesema Dkt Mwanga.