Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Nicodemus Tambo akifungua mkutano huo.jijini Arusha.Rais wa chama hicho,Henry Ngogo, akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano huo.Mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo,Salma Kilima akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha kuhusu mkutano huo

( Picha zote na Fullshangwe Blog – Arusha )

Happy Lazaro,Arusha .

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Nicodemus Tambo, amesema Serikali iko tayari kushirikiana na wataalamu wa afya ya macho katika kuimarisha huduma hizo nchini, akisisitiza umuhimu wa wadau wa sekta ya afya kuunganisha nguvu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Wataalamu wa Optometria ulioandaliwa na Chama cha wataalamu wa macho Tanzania (TOA) uliofanyika.jijini Arusha .

Tambo amesema ni muhimu kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu afya ya macho, ikiwemo umuhimu wa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara na kuepuka matumizi ya miwani bila kupimwa na wataalamu, ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kutotambua mapema matatizo ya kuona.

“Napenda kutoa.ushauri kwa wananchi kuacha tabia ya kununua na kutumia miwani bila kupimwa na wataalamu wa afya ya macho, badala yake wahakikishe wanafanyiwa uchunguzi sahihi ili kuepuka matatizo ya macho yanayoweza kusababisha upofu.”amesema Dc Tambo.

Naye Rais wa chama hicho,Henry Ngogo, amesema ni muhimu wananchi kufanyiwa uchunguzi wa macho kabla ya kutumia miwani ili kuhakikisha wanapata huduma sahihi.

Amesema kuwa ,mkutano huo unalenga kujadili changamoto zinazowakabili, kubadilishana uzoefu na kujifunza maendeleo mapya ya teknolojia yanayoweza kuboresha huduma za afya ya macho kwa jamii.

Ngogo amesisitiza umuhimu wa wataalamu kushirikiana katika kutoa huduma bora na kuhamasisha wananchi kupima macho mara kwa mara ili kubaini matatizo mapema na kupata matibabu stahiki.

Naye Mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo,Salma Kilima amesema shughuli za utoaji huduma za afya ya macho kwa jamii ni sehemu muhimu ya mkutano wa TOA unaofanyika jijini Arusha.

Salma amesema zoezi hilo limehusisha wataalamu wa optometria pamoja na wataalamu wengine wa afya ya macho, ambao wamewapatia wananchi huduma na kuwaelekeza wagonjwa wanaohitaji matibabu zaidi kwenye vituo vinavyofaa.

“Mafunzo yanayotolewa katika mkutano huo yanawawezesha wataalamu kupata ujuzi kuhusu miongozo na teknolojia mpya, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kuboresha huduma za afya ya macho nchini.”amesema Salma .

Aidha, amewahimiza wataalamu wa optometria ambao bado hawajajiunga na chama chao kufanya hivyo ili kuimarisha ushirikiano, kutetea maslahi ya kitaaluma na kukuza maendeleo ya fani hiyo nchini.

Aidha amewaonya wanaouza miwani holela bila kufanya uchunguzi wa kitaalamu wa macho, kwani vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha afya ya wananchi na kusababisha matatizo ya macho kutogundulika mapema.

“Mtu mwenye changamoto ya kuona anapaswa kufika kwa mtaalamu wa macho kwa uchunguzi kabla ya kutumia miwani, ili kubaini chanzo cha tatizo na kupata suluhisho linalofaa badala ya kujitibu mwenyewe.”amesema Salma .

Kwa upande wake Msajili Baraza la Optometria chini ya Wizara ya Afya, Sebastiano Millanzi amesema hadi sasa Baraza limesajili wataalamu 536 na linaendelea kuimarisha mifumo ya usajili na usimamizi ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Amesema wahitimu wapya wanaofaulu mitihani husika husajiliwa awali na kufanya kazi chini ya usimamizi wa wataalamu wenye sifa kwa kipindi cha mwaka mmoja katika vituo vya afya vya umma au binafsi ili kupata uzoefu wa kitaaluma.

“Nawaomba wataalamu kuzingatia maadili na mipaka ya majukumu yao, kwani kutoa huduma nje ya uwezo wa kitaaluma kunaweza kuhatarisha afya ya wagonjwa na nawaomba kushirikiana na madaktari bingwa na wataalamu wengine ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma zinazolingana na mahitaji yao.”amesema Millanzi.