Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa mradi wa ujenzi wa meli mpya ya kisasa ya MV Mwanza itakayoanza kufanya safari zake katika Ziwa Victoria na kuhudumia nchi za Afrika Mashariki zinazozunguka ziwa hilo.
Hayo yamebainika wakati wa Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) uliofanyika jijini Kisumu nchi Kenya leo Oktoba 23, 2026.
Mkutano huo uliobeba agenda mbalimbali ikiwemo ya hifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo katika Ziwa Victoria umehudhuriwa na Mawaziri kutoka nchi nane zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Maji na Mazingira wa Uganda Meja Jenerali Mstaafu Mhe. Kahinda Otafire.
Mhe. Otafire ametoa shukrani na pongezi kwa Serikali ya Tanzania kwa mradi huo wa meli ambayo ina uwezo wa usafirishaji wa abiria 1200, mizigo tani 400 za mizigo na magari 20.
Akizungumza mara baada ya mkutano huo, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa aliyeongoza Ujumbe wa Tanzania alisema fursa hiyo ya mradi wa meli inakwenda kwenye nchi zote ambazo zimepitiwa na ziwa hilo.
Itakumbukwa ujumbe wa Tanzania chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianao wa Afrika Mashairiki (anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki) Bw. Charles Kadonya ulitembelea Bandari ya Kisumu ili kubadilishana uzoefu na pia kujadili ujio wa Meli ya MV New Mwanza inayotarajia kuanza safari zake hivi karibuni katika Bandari hiyo.
Katika ziara hiyo, alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha matumizi ya Ziwa Victoria yanakuwa yale yenye kuleta maendeleo endelevu na tija kwa nchi zote wanachama huku tukihakikisha ulinzi wa mazingira.
Aidha, Katibu Mkuu huyo aliishukuru serikali ya Kenya kwa ushirikiano inaoutoa katika kuhakikisha Meli ya MV New Mwanza inaanza safari zake katika Bandari ya Kisumu.
“Katika mkutano huu tumesikia Wajumbe kutoka Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamepokewa vizuri mradi huu wa meli na tunahakikisha meli hii inafika nchi zote wanachama ili waweze kusafiri kwa urahisi kutoka eneo moja kwenda lingine, hatua hii ni mafanikio makubwa,” alisema.
Katika hatua nyingine kupitia mkutano huo limefanyika tukio la uzinduzi wa Mpango Mkakati wa namna ya kuendeleza usimamizi wa utunzaji na hifadhi endelevu ya mazingira ya Ziwa Victoria.
Nchi zinazounda Kamisheni hiyo ni Tanzania, Kenya, Uganda (ambayo ni mwenyekiti kwa sasa), Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Somalia.
