Kuimarisha usalama na usimamizi wa mabwawa kwa ushirikiano wa wadau wote wanaohusika ni muhimu kwa usalama wa jamii.
Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji Wizara ya Maji, Bi. Domina Msonge, amesema hayo Oktoba 24, 2026 ikiwa ni siku ya mwisho ya mkutano uliohusu usalama wa mabwawa.
Amesema usalama huo si jukumu la taasisi moja pekee, bali unahitaji ushirikiano wa wadhibiti, Serikali, wadau, wabunifu wa miradi na wataalamu wengine ili kuhakikisha usalama na uendelevu wa mabwawa.
Ameainisha pamoja na mengine, washiriki wamenolewa katika usalama wa mabwawa kama sehemu ya usalama wa Taifa, viwango vya kimataifa vya usimamizi wa mabwawa ya mabaki ya migodi (GISTM), utambuzi na udhibiti wa vihatarishi, ushirikishwaji wa wadau, pamoja na mbinu bora za kimataifa za ukarabati, ufungaji na ufuatiliaji wa mabwawa baada ya kufungwa.
Mkutano umewahusisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania, Jamhuri ya Watu wa China (PRC), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) , Hispania na Afrika ya Kusini.

