Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameitaka Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuharakisha mchakato wa kuanzisha taasisi kuu ya kupambana na umaskini nchini, kwa lengo la kuimarisha uratibu na ufanisi wa programu za kuinua maisha ya wananchi.Prof. Mkumbo ametoa maelekezo hayo , Oktoba 20, 2026, jijini Dodoma, wakati wa kikao na Menejimenti ya TASAF, akisisitiza umuhimu wa kutathmini programu zilizopita na kujifunza mifumo inayotumika katika nchi nyingine ili kupata suluhisho linalofaa kwa Tanzania.

Ameelekeza utafiti na mapendekezo ya mfumo huo yakamilishwe kabla ya mwisho wa mwaka 2026, ikiwemo kuchunguza uwezekano wa kuanzisha taasisi mpya au kutumia zilizopo kusimamia mapambano dhidi ya umaskini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shadrack Mziray, amesema programu za mfuko huo zinalenga kuwawezesha wananchi kuongeza kipato, kuweka akiba na kuwekeza ili kuboresha ustawi wa kaya.

Naye Mchumi Mwandamizi na Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Claudia Zambra, amesisitiza umuhimu wa kuboresha utambuzi wa kaya maskini na kuimarisha kanzidata ya hifadhi ya jamii ili kurahisisha utoaji wa huduma na misaada, hasa wakati wa majanga, na kuongeza uwezo wa kaya kukabiliana na changamoto za kiuchumi.