MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya, amesema halmashauri hiyo imetenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda, kilimo na utalii, ikiwa ni mkakati wa kukuza uchumi wa eneo hilo, kuongeza ajira na kufungua fursa mpya za biashara kwa wananchi.

Masunya alisema maeneo ya Ugwachanya na Pawaga yametengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vinavyoweza kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, yakiwemo mahindi, mpunga na bidhaa nyingine zinazozalishwa na wakulima wa wilaya hiyo.

Alisema uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao hayo utasaidia kuongeza thamani ya bidhaa kabla ya kufikishwa sokoni, huku ukifungua fursa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati kushiriki katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.

Aliongeza kuwa halmashauri hiyo pia ina maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo cha miwa na uwekezaji unaohusiana na uzalishaji wa sukari, akieleza kuwa uwekezaji huo unaweza kuchochea shughuli za kiuchumi kuanzia kwa wakulima wadogo watakaolima miwa na kuiuzia viwanda hadi kwa wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali.

Masunya alisema uwekezaji wa aina hiyo unaweza kuongeza mahitaji ya huduma za usafirishaji, malazi, chakula na biashara nyingine, hivyo kutoa nafasi kwa wananchi kunufaika na fursa zitakazotokana na uwekezaji mkubwa.

Katika sekta ya utalii, alisema halmashauri inaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa hoteli, viwanja vya michezo na viwanja vya gofu, hatua inayolenga kuongeza vivutio na huduma zitakazowavutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Alitaja eneo la Tungamalenga na maeneo ya Kihanga kuwa miongoni mwa maeneo yanayoweza kuchangia maendeleo ya miundombinu ya malazi na shughuli za michezo, akieleza kuwa uwekezaji huo unaweza kuimarisha utalii kwa kuunganisha huduma za malazi, burudani na safari za kutembelea vivutio vya asili, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Alisema uwepo wa hoteli zenye viwango tofauti, kuanzia nyumba za kulala wageni hadi hoteli za hadhi ya juu, pamoja na viwanja vya michezo, unaweza kuongeza uwezo wa Iringa kupokea wageni, wachezaji na washiriki wa matukio mbalimbali. Hali hiyo pia inaweza kuchochea ukuaji wa biashara zinazohusiana na utalii na ukarimu.

Akizungumzia changamoto zinazoweza kukabili wawekezaji, Masunya aliwataka wanaotaka kuwekeza kufika moja kwa moja katika ofisi za halmashauri ili kupata maelekezo na ushauri kuhusu maeneo yanayofaa kwa miradi yao, badala ya kutegemea watu wasiohusika rasmi katika taratibu za uwekezaji.

Alisema ofisi za halmashauri ziko wazi kwa wawekezaji wanaohitaji kufahamu taratibu za kupata ardhi, masharti ya uwekezaji na uwezekano wa kuingia katika ubia na halmashauri kwa kuzingatia sheria na mikataba inayotambulika kisheria.

Masunya alieleza kuwa ardhi ni mojawapo ya mambo muhimu katika kuanzisha uwekezaji, huku halmashauri ikiwa tayari kujadili njia mbalimbali za kuwezesha miradi, ikiwemo ubia na utoaji wa ardhi kwa masharti yanayokubalika kisheria.

Alisisitiza kuwa uwekezaji katika viwanda, kilimo, utalii na huduma nyingine ni muhimu katika kujenga uchumi unaojumuisha wananchi wengi, kuongeza ajira na kuifanya Iringa kuwa eneo lenye ushindani katika kuvutia wawekezaji na wageni kutoka maeneo mbalimbali.