Zaidi ya wananchi 200 wametembelea banda la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) katika maonesho ya kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani mkoani Tanga, kujifunza aina mbalimbali za mbegu bora, sifa zake na namna ya kuzitumia ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, alipotembelea banda hilo, Afisa Masoko wa ASA, Suzan Ludovick, amesema wananchi wamepata elimu kuhusu aina za mbegu zinazouzwa na taasisi hiyo, ubora wake pamoja na maeneo yanayofaa kwa kilimo chake kulingana na hali ya hewa.
Amesema ASA inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya mbegu zinazoweza kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mbegu ya mahindi aina ya T105, ambayo ina uwezo wa kustahimili mazingira yenye maji mengi, hatua inayoweza kuwasaidia wakulima kupunguza athari za mvua nyingi zinazoweza kujitokeza katika msimu wa kilimo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amepongeza teknolojia mbalimbali za kilimo zilizooneshwa katika maonesho hayo, akieleza kuwa matumizi ya teknolojia na mbegu bora ni miongoni mwa njia muhimu za kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi, hususan wakulima, kutumia fursa za maonesho hayo kujifunza teknolojia mpya na kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi bora katika shughuli zao za kilimo.

