Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania imezindua duka maalumu la kisasa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano, kifedha na kidijitali kwa wananchi, pamoja na kuboresha huduma kwa wateja.
Duka hilo lililopo katika jengo la makao makuu ya Airtel Tanzania limezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, likiwa na lengo la kusogeza huduma mbalimbali karibu na wateja kwa kuziweka katika eneo moja.
Huduma zinazopatikana katika duka hilo ni pamoja na intaneti, Airtel Money, intaneti ya nyuzi za mawasiliano (fibre) kwa matumizi ya nyumbani na biashara, suluhisho za kidijitali kwa kampuni na taasisi, usajili wa laini pamoja na huduma kwa wateja.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Chalamila alisema mawasiliano ya uhakika ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya biashara na ukuaji wa uchumi wa Dar es Salaam, hivyo kuipongeza Airtel kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali.
Alisema kampuni hiyo inapaswa kuendelea kuboresha huduma zake ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wananchi, huku ikihakikisha wateja wanapata huduma bora na msaada kwa wakati.
Chalamila pia aliipongeza Airtel kwa uwekezaji wake katika teknolojia za mawasiliano za 4G na 5G, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ubora wa huduma ili wananchi wanufaike na maendeleo ya teknolojia.
Aidha, alieleza umuhimu wa mchango wa Airtel katika uchumi wa taifa kupitia ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania, ambayo inamiliki asilimia 49 ya hisa za kampuni hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema uzinduzi wa duka hilo unaakisi dhamira ya kampuni ya kupanua upatikanaji wa huduma bora na kuchangia ukuaji wa uchumi jumuishi wa kidijitali na kifedha.
Kamoto alisema katika mwaka 2026, Airtel imelipa gawio la shilingi bilioni 65.48 kwa Serikali, na kufanya jumla ya gawio lililolipwa tangu mwaka 2019 kufikia takribani shilingi bilioni 350.
Aliongeza kuwa Airtel imeanzisha zaidi ya maduka 95 nchini kote, sambamba na matawi ya Airtel Money na maelfu ya mawakala, hatua inayosaidia kupanua upatikanaji wa huduma zake katika maeneo mbalimbali nchini kupitia mkakati wake wa Airtel Kila Kona.
Naye Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Airtel Tanzania, Adriana Lyamba, alisema duka hilo limebuniwa kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia za kisasa za kidijitali na utunzaji wa mazingira ili kuboresha utoaji wa huduma na kurahisisha upatikanaji wake kwa wateja.
Lyamba alisema duka hilo ni tofauti na maduka mengine ya kampuni hiyo kwa kuwa limeundwa kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa, huku likizingatia matumizi bora ya teknolojia na utunzaji wa mazingira.
Alisema Airtel inaendelea kuwekeza kwa watu, teknolojia na miundombinu ili kukidhi matarajio ya wateja na kuboresha uzoefu wao wanapotumia huduma za kampuni hiyo.
Uzinduzi wa duka hilo ni sehemu ya juhudi za Airtel Tanzania za kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kifedha, kukuza ubunifu, kusaidia shughuli za biashara na kuchangia maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Airtel Tanzania inaendelea kutekeleza kaulimbiu yake ya Airtel Kila Kona, ikiwa na dhamira ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha wanaendelea kunufaika na fursa zinazotokana na teknolojia ya kisasa.
