Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (kulia), akizungumza na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Stanbic Bank Tanzania, Jonathan Ngoma (katikati kushoto), huku Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo (katikati kulia), akishuhudia wakati wa ziara yake katika banda la benki hiyo Kariakoo, jijini Dar es Salaam, Oktoba 13, 2026. Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya kampeni ya Stanbic ya kuwafikia wafanyabiashara na kuwaelimisha kuhusu huduma ya kulipia bidhaa kutoka China moja kwa moja kwa yuan kupitia mfumo wa CIPS, bila kulazimika kubadilisha shilingi kwenda dola za Marekani kwanza.
…………..
*Stanbic yawarahisishia wafanyabiashara K’koo kulipia mzigo China
Dar es Salaam. Benki ya Stanbic Tanzania imewafuata wafanyabiashara wa Kariakoo katika maeneo yao ya biashara kuwahamasisha kutumia huduma inayowawezesha kulipia bidhaa kutoka China kwa yuan moja kwa moja kutoka kwenye akaunti zao za shilingi, hatua inayolenga kupunguza gharama za miamala na kurahisisha biashara kati ya nchi hizo.
Huduma hiyo inatumia mfumo wa malipo wa China wa Cross-Border Interbank Payment System (CIPS), unaowawezesha wafanyabiashara kulipa wasambazaji wao nchini China kwa yuan kutoka kwenye akaunti zao za shilingi bila kulazimika kubadilisha fedha hizo kwanza kuwa dola za Marekani.
Akizungumza wakati wa kuhamasisha matumizi ya huduma hiyo Kariakoo, Oktoba 13, 2026, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema kupunguza gharama za malipo ya kimataifa kunaweza kusaidia wafanyabiashara kuelekeza fedha zaidi katika kuongeza bidhaa, ajira na kukuza biashara zao.
“Serikali inataka kila biashara ya Mtanzania, kuanzia wazalishaji wakubwa hadi wafanyabiashara wa Kariakoo, ifanye biashara na dunia kwa gharama ndogo iwezekanavyo. Kila shilingi inayookolewa kwenye malipo ni shilingi inayoweza kurejeshwa kwenye bidhaa, ajira na ukuaji,” alisema.
Kapinga aliipongeza Stanbic kwa kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo yao ya kazi na kuwataka kutumia njia rasmi na zinazosimamiwa kisheria wanapolipa wasambazaji wao.
Alisema China imefungua soko lake kwa baadhi ya bidhaa za Tanzania bila ushuru, akisisitiza umuhimu wa nchi kuongeza mauzo yake katika soko hilo badala ya kutegemea zaidi uagizaji wa bidhaa kutoka China.
Kwa mujibu wa Stanbic, huduma hiyo ilizinduliwa Agosti 12, 2026, na kuifanya benki hiyo kuwa ya kwanza nchini kutoa malipo ya moja kwa moja kutoka shilingi kwenda yuan kupitia mfumo wa CIPS.
Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Stanbic Bank Tanzania, Jonathan Ngoma, alisema huduma hiyo inalenga kurahisisha biashara kwa kuwapa wafanyabiashara njia ya kufanya malipo ya kimataifa kwa urahisi zaidi.
“Kariakoo ni mojawapo ya vitovu vikubwa vya biashara nchini, kinachowaunganisha maelfu ya wafanyabiashara na wasambazaji na masoko ya kimataifa. Tumewafuata hapa ili kuwaonesha kwamba sasa wanaweza kuwalipa wasambazaji wao wa China kwa urahisi zaidi, kupunguza gharama za miamala na kuelekeza nguvu zaidi katika kukuza biashara zao,” alisema
China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Tanzania kwa miaka 10 mfululizo. Kwa mujibu wa taarifa ya benki hiyo, biashara kati ya nchi hizo ilifikia dola za Marekani bilioni 11.28 mwaka 2025, ikiwa ni mara ya kwanza kuvuka kiwango cha dola bilioni 10.
Katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2026, thamani ya biashara kati ya Tanzania na China ilifikia dola bilioni 6.48.
Sehemu ya bidhaa zinazoagizwa kutoka China, zikiwemo vifaa vya kielektroniki, nguo, vifaa vya ujenzi na bidhaa za nyumbani, hupitia Kariakoo kabla ya kusambazwa kwa wateja nchini Tanzania na nchi jirani.
Stanbic imesema malipo yanayokidhi masharti ya benki yanaweza kukamilika ndani ya dakika chache, kutegemea taratibu za kawaida za kibenki na saa za kazi.
Benki hiyo pia imesema haitatoza ada ya uhamisho wa fedha kwa malipo ya moja kwa moja ya yuan hadi Desemba 31, 2026. Huduma hiyo inapatikana katika matawi yote ya benki hiyo kwa wafanyabiashara binafsi, biashara ndogo na kampuni kubwa.
Aidha, wafanyabiashara wanaweza kutumia mikataba ya kubainisha kiwango cha ubadilishaji fedha mapema ili kupunguza athari za mabadiliko ya viwango kati ya kuagiza bidhaa na kufanya malipo.
Mkuu wa kitengo cha wafanyabiashara wadogo na wa kati, Stanbic Bank Tanzania, Fatma Ahmed, alisema huduma hiyo inaweza pia kurahisisha malipo kwa wafanyabiashara wa Tanzania wanaouza bidhaa zao nchini China.
Alisema tangu Mei 1, 2026, China imeondoa ushuru kwa bidhaa kutoka nchi 53 za Afrika, zikiwemo Tanzania, hatua inayofungua fursa kwa bidhaa za Tanzania kama ufuta, korosho, parachichi na kahawa.
“Msafirishaji anaweza sasa kupokea Shilingi moja kwa moja kwenye akaunti ya Stanbic na kujua kwa uhakika kiasi ambacho mzigo wake utazalisha kabla haujaondoka bandarini. Jukumu letu ni kuhakikisha biashara za Tanzania zinauza China kwa kujiamini kama zinavyonunua kutoka huko,” alisema
Kwa upande wake, mmiliki wa Mwangaza Home Supplies, Asha Mwakalinga, biashara ya bidhaa za nyumbani iliyopo Kariakoo, alisema huduma hiyo inaweza kupunguza changamoto za ucheleweshaji wa malipo na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha.
“Unapoendesha biashara kama yetu, bidhaa nyingi zinatoka China, hivyo kufanya malipo kwa wasambazaji ni jambo tunalolifanya mara kwa mara. Wakati mwingine mchakato huchukua muda mrefu kuliko inavyotarajiwa, na viwango vya kubadilisha fedha huathiri kiasi tunachotumia,” alisema.
Aliongeza kuwa huduma inayomwezesha mfanyabiashara kulipa moja kwa moja kwa yuan kutoka kwenye akaunti ya shilingi inaweza kurahisisha malipo na kusaidia kudhibiti gharama za uendeshaji.

