Tunduma
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Wycliffe Makamba, amesema maboresho ya miundombinu ya umeme kupitia Mradi wa TAZA yanaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Tunduma na jirani, hatua inayolenga kuongeza uhakika wa huduma hiyo na kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya wananchi.
Mhe. Salome ameyasema hayo Oktoba 15, 2026, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa TAZA katika maeneo mbalimbali.
Amesema kuwa umeme ni nyenzo muhimu katika kukuza biashara, uzalishaji na shughuli nyingine za kiuchumi, hivyo maboresho yanayoendelea kutekelezwa yatasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa umeme na kuweka mazingira bora kwa wananchi kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya umeme ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika, sambamba na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji na kufungua fursa mpya za kiuchumi.
‘Utekelezaji umefikia asilimia 92 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026. Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kutoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi wa Tunduma na maeneo jirani’ amesema Mhe. Salome
Kwa upande wake, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, amesema Wizara itaendelea kusimamia wakandarasi wanaotekeleza mradi huo ili kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati, kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na hatimaye kuwawezesha wananchi kunufaika na huduma bora na ya uhakika ya umeme.

