Afisa Mfawidhi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) , Tawi la Dar es Salaam, Shoma Philip, akizungumza na walezi wa klabu za haki za binadamu katika shule za msingi na sekondari Wilaya ya Mkuranga wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika katika wilaya hiyo Mkoani Pwani. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)

Wakufunzi wakiwajengea uwezo n walezi wa klabu za haki za binadamu katika shule za msingi na sekondari Wilaya ya Mkuranga

Baadhi ya Walezi wa klabu za haki za binadamu katika shule za msingi na sekondari Wilaya ya Mkuranga wakichangia mada wakati wa mafunzo 

Afisa Mfawidhi wa THBUB, Tawi la Dar es Salaam, Shoma Philip (katikati) pamoja na Wafanyakazi wengine wa THBUB wakiwa katika picha ya pamoja na walezi wa klabu za haki za binadamu katika shule za msingi na sekondari Wilaya ya Mkuranga

………..

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka walezi wa klabu za haki za binadamu katika shule za msingi na sekondari nchini kutumia vipawa na ubunifu kuwawezesha wanafunzi kuelewa umuhimu wa haki za binadamu ili waweze kujilinda dhidi ya ukatili na kusaidia kutoa elimu hiyo katika jamii.

Akizungumza mkoani Pwani wakati akifungua mafunzo kwa walezi wa klabu za haki za binadamu katika shule za msingi na sekondari Wilaya ya Mkuranga, Afisa Mfawidhi wa THBUB, Tawi la Dar es Salaam, Shoma Philip, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea walezi uelewa kuhusu majukumu ya Tume pamoja na mwongozo wa uendeshaji wa klabu za haki za binadamu zilizoanzishwa katika shule za wilaya hiyo.

Bi. Philip amesema mafunzo hayo ni fursa kwa walezi kupata maarifa na misingi muhimu itakayowawezesha kuendesha klabu hizo kwa ufanisi, kuwavutia wanafunzi kujiunga nazo na kuimarisha uelewa kuhusu haki za binadamu miongoni mwa watoto.

Amesisitiza kuwa haki za watoto ni sehemu ya haki za binadamu zinazopaswa kuheshimiwa na kulindwa, zikiwemo haki ya kuishi, kupata afya na elimu, kulindwa dhidi ya ukatili na kushirikishwa katika masuala yanayowahusu.

“Haki za watoto ni haki za msingi zinazomlinda kila mtu aliye chini ya umri wa miaka 18. Tume inatamani kila mwanafunzi awe mwanachama wa klabu hizi ili elimu ya haki za binadamu iweze kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na hatimaye kusambaa katika jamii nzima,” amesema Bi. Philip.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa maarifa yatakayopatikana kupitia mafunzo hayo unatarajiwa kuchochea mabadiliko chanya kwa kujenga utamaduni wa kuheshimu, kutetea na kulinda haki za binadamu kuanzia shuleni hadi katika jamii.

Kwa upande wao, walezi walioshiriki mafunzo hayo, akiwemo Mwalimu Paschal B. Ntumba na Mwajuma M. Chanzi, wameahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo maarifa waliyopata ili kuimarisha shughuli za klabu hizo na kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu haki za binadamu.

Aidha, wamewataka wadau mbalimbali kushirikiana katika kufuatilia na kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa yanayohusu watoto, pamoja na kuhakikisha watoto wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia wanapatiwa msaada stahiki kwa kushirikiana na maafisa ustawi wa jamii.

Wamesisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya haki za binadamu kwa watu wa rika mbalimbali, ikiwemo kutumia vipeperushi na njia nyingine za mawasiliano ili kuifikia jamii.