Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeazimia kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya utalii na usimamizi wa wanyamapori, ikiwemo kuoanisha sera, mifumo ya udhibiti, masharti ya utoaji wa leseni na viwango vya ubora wa huduma na kuitangaza EAC kama kituo kimoja cha utalii, ili kuongeza ushindani katika soko la sekta hiyo duniani.
Azimio hilo limefikiwa katika Mkutano wa 13 wa Baraza la Kisekta la Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori la EAC, uliofanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 15, 2026, katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.
Mkutano huo uliohitimishwa leo, Oktoba 15, 2026 katika ngazi ya mawaziri, umewakutanisha mawaziri wanaosimamia sekta ya Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori kutoka Nchi Wanachama wa EAC, kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza utalii endelevu, kuboresha ubora wa huduma na kuongeza manufaa ya kiuchumi yatokanayo na rasilimali za utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo – Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame, alisema kuwa mafanikio ya sekta ya utalii hayategemei mvuto wa rasilimali zilizopo EAC pekee, bali yanategemea ubora wa huduma zinazotolewa, uzoefu wanaopata wageni na ushirikiano wa Nchi Wanachama katika kuitangaza Afrika Mashariki kama eneo moja la utalii.
Alieleza kuwa utajiri wa rasilimali za utalii katika Nchi Wanachama unapaswa kutumiwa kama fursa ya kuongeza ushindani wa kikanda katika soko la kimataifa, kuvutia uwekezaji, kutengeneza ajira, kukuza biashara, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi.
Mkutano huo unafanyika wakati Tanzania, Kenya na Uganda zikiendelea na maandalizi ya pamoja ya kuandaa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027. Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa fursa muhimu ya kutangaza vivutio vya utalii vya nchi hizo na kuongeza umaarufu wa vivutio vya utalii vya EAC katika soko la kimataifa.
Hatua hizo pia zinatarajiwa kufungua fursa kwa hoteli, kampuni za usafirishaji, waongoza watalii, watoa huduma za chakula, wasanii na wajasiriamali wadogo na wa kati kushiriki na kunufaika na shughuli za kiuchumi zitakazochochewa na AFCON 2027.
Aidha, mawaziri walitoa wito kwa Nchi Wanachama kuharakisha utekelezaji wa maamuzi na maelekezo yaliyotolewa katika mikutano iliyopita, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa maazimio ya kikanda yanatafsiriwa kuwa matokeo yanayopimika katika sekta ya utalii na usimamizi wa wanyamapori.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame (Mb), akiambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), Naibu Waziri wa Utalii na Malikale wa Zanzibar, Mhe. Juma Hassan Thabit (Mb), pamoja na watendaji waandamizi kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.

