Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Madiwani wa Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wamemtaka mkandarasi anayetekeleza miradi ya maendeleo kupitia Programu ya TACTIC kuongeza kasi ya ujenzi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.

Agizo hilo limetolewa Oktoba 13, 2026, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Judith Mluge, wakati wa ziara ya madiwani kukagua miradi ya maendeleo katika eneo la Makaburi ya Pangani na Kata ya Tangini.

Katika ziara hiyo, madiwani wamekagua miradi inayohusisha ujenzi wa miundombinu ya soko, barabara na eneo la mapumziko na burudani (Recreation Area), inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Mluge ameeleza ni muhimu utekelezaji wa miradi hiyo kusimamiwa kwa karibu ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaboresha mazingira ya biashara, kurahisisha usafiri na kuwapatia wananchi maeneo bora ya mapumziko, hatua itakayochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Manispaa ya Kibaha.