Dodoma

Wizara ya Nishati leo imekutana na wawakilishi wa Taasisi ya African Trade and Investment Development Insurance (ATIDI), inayojishughulisha na utoaji wa bima dhidi ya hatari za kibiashara na kisiasa ambapo pande hizo mbili zimejadiliana kuhusu upatikanaji wa mitaji ili kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi katika miradi ya nishati jadidifu nchini.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Mtumba jijini Dodoma, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, amesema lengo la Serikali la kuongeza uzalishaji wa umeme hadi megawati 8,000, ifikapo 2030 linahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau binafsi ili kuharakisha upatikanaji wa kiasi hicho cha umeme.

“Lengo la Wizara ya Nishati ni kuhakikisha tunafikia megawati 8,000 za umeme. Bado tuna nafasi ya kushirikiana na ATIDI kuwezesha kampuni binafsi kutoa mchango katika kusukuma mbele ajenda ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini,” amesema Mhandisi Luoga.

Aidha, amesema ushirikiano na ATIDI unatarajiwa kusaidia kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa mitaji zinazokabili kampuni binafsi zinazokusudia kuwekeza katika miradi ya nishati jadidifu, hivyo kuongeza fursa za uwekezaji na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Serikali katika sekta ya nishati.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe kutoka ATIDI, Obbie Banda, amesema taasisi hiyo imelenga kuchangia maendeleo ya Afrika kwa kupunguza vihatarishi vya uwekezaji na kuvutia mitaji yenye gharama nafuu kupitia ushirikiano na Serikali pamoja na sekta binafsi.

“Dhamira yetu ni kuchangia maendeleo kwa kuboresha mtazamo wa wawekezaji kuhusu hatari za uwekezaji barani Afrika na kuvutia uwekezaji wenye gharama nafuu kwa kushirikiana na Serikali za nchi za Afrika na sekta binafsi,” amesema Banda

ATIDI inalenga kuwezesha biashara na uwekezaji barani Afrika kwa kutoa huduma za bima zinazopunguza hatari za kibiashara na kisiasa, hivyo kuongeza imani ya wawekezaji na wakopeshaji katika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Maafisa kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, TANESCO, REA na EWURA.