Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe.Deus Clement Sangu (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Halmashauri ya Sumbawanga Vijijini (waliokaa) pamoja na baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Rukwa wakati wa kufunga mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kupitia mradi wa DigiTruck wa Kampuni ya Huawei Tanzania wenye lengo la kuboresha ufundishaji kwa walimu nchini Tanzania.
NoWaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe.Deus Clement Sangu (Katikati) akiwa ndani ya Gari DigiTruck wakati akishuhudia baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Rukwa wakipatiwa mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kupitia mradi wa DigiTruck wa Kampuni ya Huawei Tanzania wenye lengo la kuboresha ufundishaji kwa walimu nchini Tanzania.
………
Na Mwandishi Wetu, Rukwa
Zaidi ya walimu 100 mkoani Rukwa wamenufaika na mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kupitia mradi wa DigiTruck wa Kampuni ya Huawei Tanzania, kwa lengo la kuboresha ufundishaji.
Akihitimisha mafunzo hayo Oktoba 12, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe.Deus Clement Sangu, alisema mradi huo unasaidia kupunguza pengo la ujuzi wa kidijitali na kuimarisha ubora wa elimu.
Mhe.Sangu alisema tangu kuanza nchini mwaka 2024, mradi huo umefika katika mikoa 17. Kati ya Mikoa hiyo Mkoani Rukwa, mafunzo yametolewa kwa wiki tano katika shule za sekondari za Rukwa, Katuula, Uchile na Mpui, huku yakiendelea katika Shule ya Sekondari Mzindakaya.

Alisema walimu wanapaswa kutumia maarifa hayo kuandaa masomo yenye ubunifu na kutumia teknolojia kurahisisha ujifunzaji, akibainisha kuwa hatua hiyo inaunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Waziri huyo aliipongeza Huawei kwa uwekezaji wa kijamii akiwataka walimu walionufaika kutumia na kushirikisha wenzao maarifa waliyoyapata.

Naye Meneja wa Mahusiano wa Huawei Tanzania, Boniface Leonard Ntimba, aliishukuru Serikali kwa ushirikiano na kuahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana nayo kuendeleza mradi huo nchini.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Rukwa Girls, Jane Kanyama, aliishukuru Serikali na Huawei kwa mradi huo, akisema una manufaa kwa shule na kuomba urejee tena ili walimu wengi zaidi wanufaike.

DigiTruck ni darasa linalotembea lenye kompyuta 21, ubao janja, intaneti na nishati ya jua, linalolenga kufikisha mafunzo ya teknolojia kwa wananchi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo ya vijijini.