Na Oscar Assenga,TANGA

 

Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imeeleza kwamba matumizi ya mbegu zinazokidhi viwango ni hatua muhimu katika kuwawezesha wakulima kuzalisha chakula cha kutosha na chenye ubora unaotakiwa 

 

Hayo yalisemwa na Mtafiti na Mkaguzi wa Mbegu kutoka TOSCI Aleti Kibalazo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya shule ya Sekondari Usagara kunakofanyika Maonyesho ya siku ya Chakula Duniani Jijini Tanga 

 

Ambapo alisema wameendelea kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora, ikieleza kuwa hatua hiyo ni msingi muhimu wa kuongeza uzalishaji wa mazao, kuboresha ubora wa chakula na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

 

Kibalazo amesema usalama wa chakula unaanzia kwenye mbegu bora, akisisitiza kuwa jitihada za kuongeza uzalishaji wa mazao haziwezi kufikia matokeo yanayotarajiwa iwapo wakulima hawatatumia mbegu zinazokidhi viwango vilivyowekwa.

 

Amesema Serikali imewekeza katika tasnia ya mbegu, huku TOSCI ikiendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa wingi, zinawafikia wakulima kwa urahisi na zinakuwa na gharama wanazoweza kumudu.

 

Kwa mujibu wa Kibalazo, mikakati hiyo inazingatia mambo matatu muhimu yanayojulikana kama A3, ambayo ni Availability (upatikanaji wa mbegu), Accessibility (urahisi wa kuzipata) na Affordability (uwezo wa wakulima kumudu gharama zake).

 

Ameeleza kuwa upatikanaji wa mbegu bora pekee hautoshi ikiwa wakulima wanakabiliwa na changamoto ya kuzifikia kutokana na umbali au gharama za usafiri. Kutokana na hali hiyo, TOSCI inaendelea kusajili mawakala wa kusambaza mbegu hadi vijijini ili kurahisisha upatikanaji wake na kupunguza muda pamoja na gharama ambazo wakulima hutumia kuzitafuta.

 

Aidha, amesema kuongezeka kwa upatikanaji wa mbegu bora kunatarajiwa kuwawezesha wakulima kuzipata kwa urahisi zaidi. Kuongezeka kwa upatikanaji na matumizi ya mbegu hizo pia kunaweza kuchangia kupunguza gharama, kutegemea hali ya soko na mahitaji.

 

Katika kuhakikisha wakulima wanapata uelewa wa kutosha, Kibalazo amesema TOSCI inaendelea kutoa elimu moja kwa moja kupitia maonesho na kampeni mbalimbali zinazolenga kuwahamasisha kutumia mbegu zinazokidhi viwango.

 

Amesisitiza kuwa elimu hiyo haiishii kwenye mbegu za zao moja pekee, bali inahusisha mazao mbalimbali, pamoja na miche na vipando, ili kuwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za kilimo.

 

Akizungumzia malengo ya matumizi ya mbegu bora, Kibalazo amesema kwa mwaka 2026, TOSCI imeweka makadirio ya matumizi kufikia tani 120,000, huku kiwango kilichofikiwa hadi sasa kikiwa tayari kimevuka nusu ya lengo hilo.

 

Ameongeza kuwa kwa muda mrefu, taasisi hiyo inalenga kuongeza matumizi ya mbegu bora nchini hadi kufikia tani 250,000 ifikapo mwaka 2030, hatua inayotarajiwa kusaidia kuimarisha uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula.

 

Amesema maendeleo hayo yanachangiwa na kampeni zinazoendelea za kuhamasisha matumizi ya mbegu bora, huku ushiriki wa TOSCI katika Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani ukiwa sehemu ya juhudi za kukutana na wakulima moja kwa moja, kuwapatia elimu na kuwahamasisha kutumia mbegu zinazokidhi viwango ili kuboresha shughuli zao za kilimo.