*Aeleza Mpanda itakuwa na jumla ya megawati 80 na kukidhi mahitaji ya juu ya Megawati 60 ya sasa

*Asema Wananchi kunufaika na umeme wa uhakika na kuchochea shughuli za uzalishaji

Wananchi wa Mpanda, Mkoani Katavi, wanatarajia kunufaika na upatikanaji wa umeme wa uhakika kufuatia mpango wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufunga transfoma mpya katika Mkoa wa Shinyanga ifikapo Disemba 1, 2026.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme hadi megawati 80 Mpanda hali inayotarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.

Hayo yamesemwa Oktoba 13, 2026, mkoani Katavi, na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, aliyetaka kufahamu ni lini wananchi wa Mpanda watapata umeme wa uhakika. 

Bw. Twange amesema kuwa mahitaji ya juu ya umeme kwa wananchi wa Mpanda yanakadiriwa kuwa kati ya Megawati 53 na 60. Hivyo, kuongezeka Megawati 80 baada ya kifungwa transfoma hiyo kunatarajiwa kuwezesha kukidhi mahitaji hayo na kuwa na ziada ya takribani Megawati 20.

Akifafanua zaidi, Bw. Twange ameishukuru Serikali kwa uwekezaji katika miradi ya umeme na kueleza kuwa TANESCO inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi katika maeneo mbalimbali.

“Kwanza tunaishukuru sana Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika miradi ya umeme. Makadirio ya juu ya mahitaji ya umeme kwa wananchi wa Mpanda ni kati ya megawati 53 na 60. Nawahakikishia kuwa ifikapo Disemba 1, tutakuwa tayari tumefunga transfoma ya Mva 150 itakayokuwa na uwezo wa kuwezesha kupeleka jumla ya megawati 80 za umeme,” amesema Bw. Twange.

Utekelezaji wa hatua hiyo unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mji wa Mpanda na kusaidia shughuli za uzalishaji, biashara na huduma za kijamii, ambazo zinategemea nishati ya umeme.