Mwamvua Mwinyi, Kibiti
Oktoba 12,2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Mkoani Pwani Ramadhan Kimara, amesisitiza umuhimu wa kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati, akiwataka mafundi na wasimamizi kuhakikisha kazi zinafanyika kwa kuzingatia muda uliopangwa na matumizi sahihi ya vifaa vya ujenzi.
Kimara ameyasema hayo Oktoba 12, 2026, wakati akikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkupuka yenye thamani ya Sh milioni 528, iliyopo Kijiji cha Mkupuka wilayani Kibiti.
Akiwa katika eneo la mradi, amezungumza na fundi pamoja na msimamizi wa ghala la vifaa vya ujenzi, akiwataka kuhakikisha vifaa vinatumika kwa usahihi na kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akimtaka fundi kukamilisha kazi ndani ya muda uliowekwa kwenye mkataba.
Aidha Kimara amemtaka Mhandisi wa mradi kutembelea eneo la ujenzi mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya kazi na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Mjulisheni Mhandisi wa mradi ahakikishe muda wote anafika katika eneo la ujenzi ili kusiwe na changamoto zozote katika ujenzi huu,” alieleza Kimara.
Akiwa Kijiji cha Nyamisati, Kata ya Salale, kutembelea Kiwanda cha Samaki na kukagua miundombinu iliyopo pamoja na kubaini changamoto zinazokikabili.
Ukaguzi huo ulilenga kujionea hali ya kiwanda na changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kuwezesha uwekezaji huo kuanza au kuimarisha shughuli za uzalishaji, kwa lengo la kuongeza mapato ya Halmashauri na kuchochea shughuli za kiuchumi wilayani Kibiti.

