Mkuu wa Wilaya ya Arusha ,Nicodemas Tambo akizungumza kwenye halfa hiyo jijini Arusha leo

 Mkandarasi wa mradi huo,Zeng Qiang (Peter) akisaini mkataba huo jijini Arusha leo.

……………… 

Happy Lazaro, Arusha

Arusha.Mkuu wa Wilaya ya Arusha ,Nicodemas Tambo amesema uwekezaji katika ujenzi wa barabara ya Kwa Giriki hadi Mathias Manga kata ya Sakina utaongeza thamani ya mali na kuboresha maisha ya wananchi, akieleza kuwa miundombinu bora inaweza kuongeza thamani ya nyumba na mapato ya wamiliki kupitia kodi ya pango.

Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati wa uwekaji saini wa mradi huo kati ya halmashauri ya jijini la Arusha na Mkandarasi wa kampuni ya kichina ya Jiangxi Geo-Engineering Group Corporation Ltd.

Mradi huo utakajengwa kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilometa 1.5 kwa gharama ya shs milioni 950 .

Amesema nyumba iliyokuwa ikipangishwa kwa Shilingi 30,000 inaweza kufikia Shilingi 50,000 hadi 60,000 kutokana na kuboreka kwa miundombinu na kuongezeka kwa thamani ya eneo husika, huku barabara bora zikirahisisha shughuli za biashara na safari za kila siku za wananchi.

Tambo amempongeza Mstahiki Meya pamoja na Baraza la Madiwani kwa kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo, huku akieleza kuwa atafanya ziara ya kukagua miradi ambayo haijakamilika ili kubaini changamoto na sababu za ucheleweshaji.

 Amesisitiza kuwa wakandarasi wanapaswa kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Sakina, Hillary Mollel, amesema wananchi wamefurahishwa na kasi ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 1.1, akibainisha kuwa ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili, mradi huo umeonyesha maendeleo makubwa yaliyowashangaza wakazi wa kata hiyo.

Mollel amesema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wananchi, huku akieleza kuwa uwepo wa taa za barabarani umeleta mabadiliko katika mwonekano wa Sakina na kuongeza mwanga katika eneo hilo. 

Mollel amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na Mbunge wa eneo hilo ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, kwa kuendelea kuwa karibu na wananchi.

Amesema wananchi wa Sakina wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na weledi, huku akieleza kuwa wameandaa zawadi maalumu kwa mgeni rasmi kama ishara ya heshima na shukrani kwa ziara yake na juhudi za kuendeleza eneo hilo.

Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi huo,Zeng Qiang (Peter) amesema watahakikisha ujenzi wa kilomita 1.5 zilizobaki unakamilika ndani ya muda uliopangwa kwa kuzingatia viwango vya ubora, ili kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo.

Amesema pia wanatarajia kujenga barabara ya zege itakayowezesha magari kupita kwa urahisi kutoka Barabara ya Nairobi kuelekea Barabara ya Sakina .

Ameongeza kuwa, watatumia uzoefu wa zaidi ya miaka 20 walioupata katika kutekeleza miradi mbalimbali nchini Tanzania na maeneo mengine ili kuhakikisha miundombinu inayojengwa ni imara na yenye kudumu.