Mwenyekiti wa uchaguzi akiwa katika picha ya pamoja na wasimamizi na mawakala mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa kupata viongozi wapya kwa kipindi cha miaka 5 uliofanyika jijini Dodoma
…………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Chama cha klabu ya waandishi wa Habari kanda ya kati (Dodoma),Cetral Press Club (CPC) kimefanya uchaguzi na kupata viongozi wapya kwa kipindi cha miaka 5.
Akitangaza matokeo hayo leo jijini Dodoma ,Mwenyekiti wa Uchaguzi huo ,Abubakari Famau ,Mwaandishi wa Shirika la utangazaji Uingereza (BBC) amesema mwenyekiti mpya ni Mussa Yusufu kutoka Uhuru Media,huku nafasi ya makamu mwenyekiti ikichukuliwa na Mbashiru Katare kutoka Kampuni ya Magazeti Ya Serikali TSN.
Katibu mkuu mpya ni Benchine Bango mwandishi wa kujitegemea na katibu Msaidizi Musa Enock kutoka Afm Radio huku nafasi ya wajumbe ikichukuliwa na watu watatu ambao ni Jasmine Shamwepu kutoka ABM radio,Doto Kwilasa kutoka gazeti la jamvi la Habari pamoja na Amani Mbando kutoka Daily News Digital.
Naye Mwenyekiti Mteule wa CPC Mussa Yusuph amesema”Kwanza kabisa natoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwingi wa rehema aliyetujaalia sote kwa pamoja kujumuika kwenye mchakato mzima wa uchaguzi kisha kutuvusha tukiwa na amani, umoja, furaha na upendo. Hakika hilo ndio jambo jema kwetu sote.
Pili, shukrani zangu za kipekee kwenu wanachama wenzangu kwa imani kubwa mlioionyesha kwetu wagombea wote watatu, mimi, Magnus Mahenge na Daniel Mkate, hakika naimani mmetuamini sana kama ilivyojidhihirisha imani yenu kwenye mchakato mzima wa kura zilizopigwa.
Kwa dhati ya moyo wangu wagombea wenzangu, Magnus Mahenge na Daniel Mkate, ni kaka zangu wa karibu na nimejifunza na nitaendelea kujifunza mengi kutoka kwao, hivyo basi naahidi kuendelea kuchota busara na mawazo yao mazuri kwa mustakabali wa maendeleo ya CPC.
Ndugu wanachama wenzangu, imani yenu kubwa mlioionyesha kwangu, hilo ni deni ambalo ninapaswa kulilipa iwe kwa jasho, damu, machozi, mchana au usiku lazima niwatumikie kwani mimi kwenu sio kiongozi bali mtumishi wenu ninayepaswa kuwatumikia.
Yapo mengi niliyoahidi na zipo ahadi zingine za viongozi wenzangu wateule, zote kwa pamoja lazima tuzitimize pasi na ubabaifu wa aina yeyote, hivyo basi viongozi wenzangu nao wanapaswa kufahamu deni tunalopaswa kulilipa na tunapaswa kufahamu CPC sio mahali pa kuvimbisha matumbo yetu.
Jukumu letu kubwa ni kurejesha imani kwa wanachama, kukifanya chama kiwe mikononi mwa wanachama, wanachama wajivunie na kile tutakachokitekeleza na kamwe viongozi tusigeuke magwiji wa kujimwambafai, viburi, jeuri, kutosikiliza na kutotatua changamoto zinazowakabili wanachama kwa wakati muafaka.
Ndugu wanachama wenzangu, kwa hayo machache nashukuru moyo wenu wa upendo kwangu na kwa viongozi wenzangu wateule, kwa niaba yao tunaahidi kuchapakazi kwa maslahi yenu”amesema.
Katika uchaguzi huo jumla ya kura 63 zimepigwa na zilizoharibika ni 8 ambapo Mwenyekiti wa Uchaguzi huo Abubakari Famau akizungumza na mtandao huu amewashukuru viongozi wapya waliochaguliwa huku akiwataka kufanya mapinduzi makubwa ndani ya chama hicho cha Waandishi wa Habari.
Naye ,Mwenyekiti Mstaafu wa CPC Habel Chidawali kutoka Gazeti la Mwananchi ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wapya walioshinda.
“Kwa dhati ya Moyo wangu nawapongeza nyote mlioshinda na kutangazwa na mlioshinda lakini kura hazikutosha,mchuano hakukuwa cha mtoto na hata waliobeza mfumo wameona demokrasia iliyotamalaki,ahsante Famau na timu yako Mungu awabariki”amesema Chidawali.
Naye ,Aliyekuwa anagombea nafasi ya Mwenyekiti Bw.Daniel Mkate kutoka EATV amewapongeza washindi pamoja na wapiga kura wote waliompigia ila kura hazikutosha
”Ahsanteni kwa wale mliothubutu kunipigia kura na wale ambao hamkunipigia Mungu awabariki wote tusonge mbele tuijenge CPC Mawazo yetu yanatosha kukiweka chama Salama”amesema Mkate
Matokeo pamoja na kura zote kama inavyoonekana hapo chini