Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha wakulima wa Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine nchini wanapata mbolea kwa wakati katika msimu huu wa kilimo.

Silinde ametoa maelekezo hayo alipotembelea banda la TFRA wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga.

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji wa mbolea katika maeneo yote nchini ili kuwawezesha wakulima kupata pembejeo hizo kwa wakati, kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Akizungumza katika maonyesho hayo, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TFRA, Stephano Mfugale, amewahimiza wakulima kutumia mbolea sahihi na kufuata maelekezo ya matumizi yake ili kuongeza uzalishaji na kupata mavuno mengi katika eneo dogo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa mbolea za ruzuku mkoani Tanga, Hatibu Kilenga, amesema mkoa huo una mbolea za ruzuku za kutosha, huku akiwahimiza wakulima kuhakikisha wamesajiliwa katika mfumo wa ruzuku ili waweze kununua mbolea kwa utaratibu uliowekwa na Serikali.

Kilenga amesisitiza kuwa usajili sahihi katika mfumo huo ni muhimu kwa wakulima wanaotaka kunufaika na mpango wa ruzuku ya mbolea na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo hizo.

TFRA inaendelea kutekeleza jukumu lake la kusimamia upatikanaji na ubora wa mbolea nchini ili kuongeza tija katika kilimo na kuchangia usalama wa chakula, sambamba na kaulimbiu ya “Ubunifu wa Leo, Lishe Bora Kuelekea Dira ya 2050.”