Na Oscar Assenga,TANGA

WAKALA wa Taifa wa Huduma ya Ugani nchini (NAESA) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imejiandaa kutoa mafunzo kwa maafisa ugani katika mikoa 14 inayopata misimu miwili ya mvua.

 Ambapo aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Kanda ya Ziwa Victoria,Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ,Pwani ya Kaskazini na Kaskazini mwa mikoa ya Morogoro na Kigoma ili kuwajengea uwezo wa kutafsiri taarifa hizo na kuwafikishia wakulima kwa wakati.

Hayo yalisemwa leo na Kaimu Meneja wa Sehemu ya Masoko na Uongezaji wa Thamani wa Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani nchini Ester Mwaisango katika maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani ambapo kitaifa inafanyika kwenye viwanja vya Usagara Jijini Tanga.

“Wakala tumeendaa mafunzo haya kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na tunaamini watakuwa na tija kwa maafisa ugani ili kuwafikisha wakulima taarifa kwa wakati.

Mwaisango alisema kwamba wakala huo pia unasimamia shughuli mbalimbali zinazofanywa na maafisa ugani ikiwemo usajili waa wakulima katika mifumo rasmi,ambapo hadi sasa zaidi ya wakulima Milioni 5.5 wamesajiliwa na zoezi hilo linaendelea

Alisema majukumu yao pia ni kuratibu na kusimamia huduma za ugani kilimo nchini ,kusimamia na kuratibu vyuo vya mafunzo ya kilimo na vituo vya mafunzo kwa wakulima ikiwemo huduma za zana za kilimo.

Aidha aliongeza jambo jingine ni kuhamasisha kilimo biashara,kuandaa miongozo ya ufundishaji na kushirikiana na vyuo vya kilimo katika kuboresha mitaala inayotumika kutoa elimu kwa maafisa ugani .

Katika Maadhimisho hayo Naesa imeshiriki ikiambatana na wawakilishi kutoka vyuo vinavyotoa mafunzo ya uhaulishaji wa teknolojia za kilimo,

Wawakilishi hao wakiwemo wakufunzi ,wameelezea teknolojia mbalimbali zinazofundishwa kwa maafisa ugani ,miongoni mwa teknolojia hizo ni uchakataji wa mpungga kwa kutumia mvuke kabla ya kukobolewa unaolenga kuboresha ubora wa mchele na kupunguza upotevu.

Akizungumza teknolojia hiyo,Hamisi Ramadhani kutoka Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Ulenga kilicho chini ya NAESA alisema wameona umuhimu wa kuwafundisha wakulima mbinu zinazoweza kuongeza tija na mapato yao.

Alisema wakulima wengi wamekuwa wakiuza mpunga wakiwa shambani au kupeleka katika mashine za kawaida za kukoboa hali inayoweza kuwanyima fursa ya kuongeza thamani ya mazao yao na kunufika zaidi na kilimo wanachokifanya ,

Ramadhani alisema kupitia teknolojia ya kutumia mvuke katika uchakataji wa mpunga,wakulima wanaweza kuboresha ubora wa mchele na kupunguza kiasi cha mchele kinachovunjika wakati wa kukobolewa.

Aliongeza kwamba lengo ni kuhakikisha wakulima wanapata maarifa na teknolojia zitakazowasaidia kuongeza thamani ya mazao yao,kupanua fursa za masoko na kuongeza kipato kutokana na kilimo.

Alisema juhudi hizo zinaendana na msisitizo wa NAESA kuhusu maarifa ,ubunifu na tija,kwa kuhakikisha wakulima wanatumia mbinu bora za uzalishaji na uchakataji ili kilimo kiwe na manufaa zaidi ya kiuchumi