Na.Sophia Kingimali- Dar Es Salaam
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeweka mikakati mipya ya kuongeza urejeshaji wa mikopo inayodaiwa kufikia takribani Sh800 bilioni, ikiwalenga zaidi wanufaika walio katika sekta isiyo rasmi ili kuhakikisha fedha hizo zinaendelea kutumika kufadhili wanafunzi wengine.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, amesema hayo leo Oktoba 12, 2026, katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika Dar es Salaam, akieleza mafanikio ya bodi hiyo katika kipindi cha miaka mitano na hatua zinazochukuliwa kuimarisha uendelevu wa ufadhili wa elimu ya juu.
Amesema changamoto ya ajira na kutokuwa na kipato cha uhakika kwa baadhi ya wahitimu imeifanya bodi kubuni mbinu zinazowawezesha wanufaika kurejesha mikopo kwa kuzingatia uwezo wao wa kifedha, huku ikiendelea kuimarisha mifumo ya kuwafikia wadaiwa.
Aidha Dk. Kiwia amesema, kuanzia mwaka wa fedha 2005/2006 hadi Juni 2026, HESLB imekusanya Sh1.91 trilioni kati ya Sh2.77 trilioni za mikopo iliyofikia muda wa kurejeshwa, sawa na ufanisi wa asilimia 69.
Amesema makusanyo yameendelea kuongezeka, kutoka takribani Sh177 bilioni mwaka wa fedha 2023/2024 hadi Sh194 bilioni mwaka 2024/2025, kabla ya kufikia Sh235.5 bilioni mwaka 2025/2026.
Ameeleza kuwa makusanyo ya mwaka wa fedha 2025/2026 yalifikia asilimia 107 ya lengo la Sh220 bilioni, hatua inayoonesha ongezeko la fedha zinazorejeshwa kwa ajili ya kuendeleza mpango wa mikopo ya elimu ya juu.
Katika kuhakikisha ufadhili huo unawafikia wanafunzi wengi zaidi, Serikali imetenga Sh1.06 trilioni kwa mwaka wa masomo 2026/2027, zitakazotumika kugharimia wanafunzi wasiopungua 300,000, kutoka Sh916.7 bilioni zilizotengwa mwaka uliotangulia.
Dk. Kiwia amesema katika mwaka wa masomo 2025/2026, wanafunzi 289,932 walinufaika na mikopo, huku bajeti ya mwaka huu ikiongezeka kwa asilimia 15.6, hatua inayolenga kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu.
Akitaja utekelezaji wa ufadhili kwa mwaka huu, amesema awamu ya kwanza iliyotangazwa Oktoba 10, 2026, ilihusisha wanafunzi 165,775 waliopangiwa mikopo na ruzuku zenye thamani ya Sh535.7 bilioni.
Amesema kati ya wanafunzi hao, 74,769 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali wamepangiwa Sh246.88 bilioni, wanafunzi 8,538 wa stashahada Sh22.9 bilioni, huku wanafunzi 873 wakipangiwa ruzuku ya Sh4.5 bilioni kupitia Samia Scholarship.
Kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo, amesema 79,115 wamepangiwa mikopo ya Sh252.4 bilioni, wanafunzi 1,554 wa stashahada Sh3.8 bilioni na wanufaika 926 wa Samia Scholarship wakipangiwa ruzuku ya Sh5.1 bilioni.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano, bodi imepanua wigo wa ufadhili kwa kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada mwaka wa masomo 2023/2024, sambamba na kuongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza kutoka Sh8,500 hadi Sh10,000 kwa siku.
Katika kuboresha huduma, HESLB imeimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali ikiwemo OLAMS, SIPA, HESLB App na DiDiS, pamoja na mifumo saidizi ya akili unde ya Bwanaboom na Bibiboom inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na majibu kuhusu huduma za mikopo.
Naye Mkurugenzi wa Urejeshaji na Urejeshwaji wa Mikopo wa HESLB, CPA George Mziray, amesema bodi inaendelea kutumia kampeni za #Fichua na #Kiduchu Fresh Tunasonga kuongeza makusanyo na kuwahamasisha wanufaika kutimiza wajibu wao wa kurejesha mikopo.
Amesema kampeni ya #Kiduchu Fresh Tunasonga inalenga kuwapa nafasi wanufaika wenye kipato kidogo kuanza kurejesha mikopo yao kwa kiasi kinacholingana na uwezo wao, hususan wale wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi.
Awali, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Sabato Kosuri, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kuelimisha umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi za umma kwa kutoa taarifa sahihi zinazochochea uwazi, uwajibikaji na ushirikiano kati ya taasisi hizo na wananchi.

