Mkuu wa shule hiyo, Augustino Lubuva akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha leo
Happy Lazaro, Arusha.
ARUSHA: SHULE ya mchepuo wa kiingereza ya Albehije iliyopo jijini Arusha, imeeleza namna elimu jumuishi inavyoweza kuwapa watoto wenye ulemavu nafasi ya kujifunza, kukuza vipaji na kujiandaa kujitegemea pamoja na watoto wengine.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa shule hiyo, Augustino Lubuva katika mahafali ya 16 ya wanafunzi wa elimu ya awali na msingi ambapo amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikipokea wanafunzi kutoka mazingira mbalimbali, wakiwemo wenye mahitaji maalumu, na kuwaweka katika mazingira yanayowawezesha kushiriki kikamilifu katika masomo.
Amesema kuwa,baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu waliojiunga na shule wakiwa na changamoto za kusikia, kuzungumza au kutembea wameweza kusonga mbele kielimu kutokana na fursa ya kupata elimu katika mazingira jumuishi.
“Mbali na elimu jumuishi, shule yetu imekuwa ikisisitiza nidhamu pamoja na malezi, ikiamini kuwa mafanikio ya mtoto hayaishii katika ufaulu wa darasani pekee, bali yanahitaji kujengwa kwa misingi ya maadili na uwajibikaji.”amesisitiza Lubuva .
Kwa upande wa taaluma, amesema wanafunzi wameendelea kufanya vizuri katika mitihani, huku wanafunzi wa Darasa la Nne wakitajwa kupata madaraja A na B, na wale wa Darasa la Saba kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kitaaluma.
Lubuva amesema kuwa,shule imeanza kuwajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo kupitia mtaala unaozingatia elimu ya amali, ukiwemo ufugaji, ushonaji, kilimo, uhandisi na ufundi mbalimbali, ili kuwawezesha kuwa na uwezo wa kutumia maarifa yao nje ya darasa.
“Elimu hiyo ya vitendo inalenga kuhakikisha mtoto anapomaliza elimu ya msingi anakuwa na ujuzi wa ziada unaoweza kumsaidia katika maisha na kumjengea uwezo wa kujitegemea.”amesema Lubuva .
“Mfumo huo umeendelea pia katika shule yetu ya Albehije Secondari iliyopo Wilaya ya Arumeru, ambako wanafunzi wanaweza kuendelea na masomo katika mazingira yanayochanganya taaluma na ujuzi wa vitendo.”amesema Lubuva.
Lubuva amesema kuwa,katika.shule hiyo ya sekondari Albehije ambayo ni shule ya kutwa na bweni mbali na kutoa masomo ya kawaida pia shule hiyo inatoa kozi za ushonaji na teknolojia ya nguo,uongozi wa utalii na usafiri,sayansi ya kompyuta na lugha ya kifaransa,hivyo amewataka wazazi kuchangamkia.fursa hiyo kwa kupeleka watoto wao katika shule hiyo kutokana na utofauti walio nao.
Aidha amewataka wazazi kutambua kuwa jukumu la malezi halimaliziki mtoto anapohitimu Darasa la Saba, hivyo wazazi wanapaswa kuendelea kuwafuatilia, kuwaongoza na kuhakikisha wanaendelea na elimu ya sekondari.
“Wazazi sasa ndio wakati wao wa kuhakikisha watoto wanasimamiwa. Wakirudi mikononi mwa wazazi, wasiachwe holela, bali wazazi wafuatilie wanachofanya na kuhakikisha wanaendelea na masomo,” amesema Lubuva.
Lubuva amesema ushirikiano kati ya shule, wazazi na jamii ndio msingi wa kuhakikisha watoto wanatumia vizuri elimu na vipaji walivyopewa, huku akiwahimiza wazazi kuwaandikisha watoto wao katika shule ya sekondari Albehije au shule nyingine zitakazowawezesha kuendelea na safari ya elimu.”amesema.
Naye mgenirasmi katika mahafali hayo Afisa Mthibiti Ubora wa Elimu wa wilaya ,Arusha Dc,Asia Mbowe amewataka wahitimu.hao kuitumia vizuri elimu waliyoipata kwa ajili ya maisha yao ya baadaye na kuweza kufikia ndoto zao.
“Nimeona namna ambavyo shule hii inafundisha vizuri na kuweza kuwaaandaa watoto kujitegemea nawaomba sana watoto wakakiendeleze kile walichofundisha hapa shuleni na kuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii huku wakiwa mabalozi wazuri wa shule hii.” amesema Mbowe.
Mmoja wa wahitimu hao, Brighton Urio, amesema Albehije imekuwa sehemu muhimu katika kuwajengea watoto wenye ulemavu uwezo wa kujiamini, kujitegemea na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kielimu.
