Na. Neema Mtuka, Sumbawanga 

Rukwa :Wananchi Mkoani Rukwa wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika kilele cha mbio za mwenge zitakazofanyika tarehe 14 oktoba,2026 katika uwanja wa Nelson Mandela Sumbawanga Mkoani Rukwa.Akizungumza na waandishi wa habari  tarehe 12 Oktoba,2026 katika ukumbi wa Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.Joel Arthur Nanauka (MB) Waziri wa nchi,ofisi ya Rais- Maendeleo ya Vijana akiwa ameambatana na Mh.Ali Suleiman Ameir Waziri wa Kazi Ajira, Vijana na uwezeshaji wa serikali ya mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Nanauka amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 zimekaribia kilele chake baada ya kupita katika halmashauri 195 na mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku ikizindua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.

“Mwenge umekagua ,umeweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo iliyokamilika”.Amesema Nanauka.

Mwenge huo ulizinduliwa rasmi tarehe 2 April 2026, na mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi, na tangu kuzinduliwa kwake, Mwenge umekuwa ukizunguka nchi nzima ukikagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi ya miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji, barabara na nyinginezo.

Mbio za mwaka huu zinafanyika wakati Taifa likiwa katika kumbukizi ya miaka 27 bila Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alifariki dunia tarehe 14 Oktoba 1999. 

Kumbukizi hiyo imekuwa ikiongozwa na kauli mbiu ya kuendeleza amani, umoja na maendeleo aliyoyasisitiza Mwalimu Nyerere.

Nanauka amesema Ibada ya misa takatifu ya kumbukizi ya miaka 27 bila baba wa taifa itafanyika katika kanisa kuu la Mt.Epifania Jimbo Katoliki Sumbawanga.

Sambamba na Mbio za Mwenge, Wiki ya Vijana Kitaifa imeanza rasmi tarehe 08 Oktoba 2026 na kuzinduliwa tarehe 10 Oktoba 2026 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba.

Aidha wiki ya vijana kitaifa iliyoanza oktoba 08 katika viwanja vya shule ya msingi Ndua Manispaa ya Sumbawanga itafikia kilele chake tarehe 14 oktoba 2026.

Wiki hiyo inalenga kuwawezesha vijana kiuchumi, kielimu na kiteknolojia, sambamba na kuwashirikisha katika shughuli za maendeleo ya Taifa.

Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 kinatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Nelson Mandela, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.