Cooperative Bank Tanzania Plc (Coop Bank) imeimarisha dhamira yake ya kuendeleza uchumi wa ushirika nchini na barani Afrika kupitia ushirikiano wa kimkakati na Shirikisho la Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Afrika (ACCOSCA) pamoja na Chama Kikuu cha Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), katika kuunga mkono SACCA Congress 2026 inayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 11 hadi 16, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah, alisema ushiriki wa benki hiyo katika kongamano hilo unatokana na nafasi yake ya kipekee kama taasisi ya kifedha inayomilikiwa kwa asilimia 51 na vyama vya ushirika, hivyo dhamira yake ya kukuza na kuimarisha sekta ya ushirika ni sehemu ya msingi wa biashara yake.

Alieleza kuwa ushiriki huo ni zaidi ya udhamini, kwani unalenga kufungua fursa za ushirikiano, kubadilishana maarifa na kuwasilisha suluhisho za kifedha zitakazowezesha Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOs) kuimarika kiutendaji, kupanua huduma zao na kuongeza thamani kwa wanachama wanaowahudumia.

“Coop Bank inaamini kuwa SACCOs imara ni nguzo muhimu katika kujenga uchumi wa ushirika wenye tija na jumuishi. Kupitia ushirikiano huu, tunalenga kuendelea kuwa mshirika wa kimkakati wa SACCOs kwa kuwapatia suluhisho za kifedha zinazowawezesha kukua, kuongeza ufanisi na kuwahudumia wanachama wao kwa ubora zaidi,” alisema Ng’urah.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SCCULT, Hassani Mnyone, alisema maandalizi ya kongamano hilo yamekamilika, akibainisha kuwa SACCA Congress 2026 ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya ushirika kutoka maeneo mbalimbali ili kujadili changamoto, kubadilishana uzoefu na kuibua mikakati mipya ya kuimarisha maendeleo ya SACCOs.

Aliongeza kuwa kongamano hilo litatoa fursa ya kujadili masuala muhimu yanayohusu upatikanaji wa huduma za kifedha, matumizi ya teknolojia, uongozi bora, uendelevu wa taasisi na ubunifu unaoweza kuongeza ushindani na ufanisi wa vyama vya ushirika.

Kupitia ushiriki wake katika SACCA Congress 2026, Coop Bank inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwa mshirika wa maendeleo ya vyama vya ushirika kwa kuunganisha huduma za kifedha na mahitaji halisi ya SACCOs, huku ikichangia kujenga taasisi imara zinazoweza kukuza ustawi wa wanachama na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.