Na Sophia Kingimali

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema Kamati ya Sera ya Fedha imeamua kuendelea kushikilia kiwango cha riba ya Benki Kuu (CBR) kuwa asilimia 6.25 kwa robo mwaka inayoishia Desemba 2026, hatua inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumza leo, Oktoba 8, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akitangaza uamuzi wa Kamati hiyo, Tutuba amesema sera ya fedha inayotekelezwa inaendelea kupenya katika uchumi na kusaidia kudhibiti shinikizo la mfumuko wa bei, huku makadirio yakionesha kuwa mfumuko huo utaendelea kubaki ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 3 hadi 5.

Amesema uamuzi huo umezingatia pia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mivutano ya kijiografia katika Mashariki ya Kati, pamoja na uwezekano wa changamoto zinazohusiana na hali ya hewa ya El Niño, ambazo zinaweza kuathiri mnyororo wa usambazaji na bei za bidhaa.

Tutuba amesema uchumi wa dunia unaendelea kukabiliwa na changamoto kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati, unaoathiri shughuli za kiuchumi, minyororo ya usambazaji wa bidhaa na jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei, hali iliyosababisha makadirio ya ukuaji wa uchumi duniani kushushwa.

Aidha, Gavana Tutuba amesema Shirika la Fedha Duniani (IMF) linakadiria uchumi wa dunia kukua kwa takribani asilimia tatu mwaka 2026, kutoka makadirio ya awali ya asilimia 3.5, huku Benki ya Dunia ikishusha makadirio yake hadi asilimia 2.5 kutoka asilimia 2.9.

Akizungumzia uchumi wa ndani, Tutuba amesema Tanzania Bara iliendelea kuonesha kasi nzuri ya ukuaji, ambapo uchumi ulikua kwa asilimia sita katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 na unatarajiwa kukua kwa zaidi ya asilimia sita katika robo ya pili na ya tatu, ukichochewa na huduma za kifedha, uzalishaji viwandani, uwekezaji katika miundombinu na huduma za kijamii.

Alisema uchumi wa Zanzibar nao ulikua kwa asilimia 6.7 katika robo ya kwanza ya mwaka huu na unatarajiwa kuvuka asilimia saba katika robo ya pili na ya tatu, ukichochewa zaidi na shughuli za utalii, ujenzi na miradi ya umwagiliaji inayoendelea kutekelezwa.

Tutuba amesema mfumuko wa bei Tanzania Bara ulifikia asilimia 4.3 Agosti 2026, kutoka wastani wa asilimia 4.1 katika robo iliyoishia Juni mwaka huo, na bado ulikuwa ndani ya wigo unaolengwa, licha ya shinikizo la bei za mafuta katika soko la dunia.

Kwa upande wa Zanzibar, amesema mfumuko wa bei ulifikia asilimia 5.6 Agosti 2026, kutoka asilimia sita Julai, hali ambayo imeifanya BoT kuendelea kuchukua hatua kuhakikisha mfumuko huo unadhibitiwa na kubaki katika kiwango kinachokubalika.

Katika sekta ya fedha, Gavana amesema mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kukua kwa kasi na kufikia wastani wa asilimia 22.5 katika robo iliyoishia Septemba 2026, akieleza kuwa ukuaji huo unaonesha kuongezeka kwa mahitaji ya mikopo kutoka kwa wananchi na wafanyabiashara.

Amesema sekta ya benki imeendelea kuwa imara na yenye uwezo wa kustahimili misukosuko, ikisaidiwa na mitaji imara na faida endelevu, huku mikopo chechefu ikiwa asilimia 2.5 Agosti 2026, kiwango ambacho kiko chini ya ukomo wa asilimia tano unaokubalika.

Tutuba amesema akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha, ikiwa zaidi ya dola bilioni sita na kuwezesha nchi kugharamia uagizaji wa bidhaa kwa takribani miezi 4.3, wakati nakisi ya akaunti ya kawaida ilifikia asilimia 2.5 ya Pato la Taifa katika mwaka ulioishia Septemba 2026.

Amesema BoT itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mzozo wa Mashariki ya Kati, athari za El Niño na viashiria vingine vya uchumi, huku ikiwa tayari kuchukua hatua kwa kutumia zana za sera ya fedha endapo shinikizo la mfumuko wa bei litaongezeka. Uamuzi mwingine kuhusu kiwango cha CBR unatarajiwa kutangazwa Januari 7, 2027, baada ya kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha cha Januari 6.